Mtayarishaji

Morning Star Radio

Jumamosi, Septemba 10, 2011

Dhambi ya asili

Wakristo wa madhehebu mbalimbali wanaita hivyo dhambi ya kwanza ya watu ambayo imekuwa asili ya dhambi zote (Rom 5:12) na ya uharibu wa dunia (Rom 8:19-25).

 
Michelangelo alivyochora katika kuta za Cappella Sistina huko Vatikano dhambi ya Adamu na Eva na adhabu iliyofuata ya kufukuzwa bustanini.


Dhambi ya Asili katika Biblia

Kitabu cha Mwanzo sura ya 3 inasimulia dhambi hiyo. Kwa njia ya hadithi hiyo tunaambiwa hali yetu mbaya haitokani na Mungu, bali na uasi wetu na wa wazee wetu (Hek 2:23-24). Pia tunafundishwa kukataa toka mwanzo vishawishi vyetu tukiamini maagizo yote ya Mungu yametolewa kwa upendo mkuu.
Shetani ndiye aliyeanzisha kishawishi. Eva alipaswa asimsikilize. Kosa lake la kwanza ni kumjibu: hivyo shetani akamdanganya kwamba, eti Mungu ana kijicho, hataki watu walingane naye, ndiyo sababu aliwakataza (Yoh 8:44). Tukianza kuzingatia kishawishi tunakubali shaka juu ya wema wa Mungu kwetu katika kutuelekeza. Kwa namna hiyo walianguka watu wa kwanza waliokuwa watakatifu; kwa urahisi zaidi tutaanguka sisi wenye tabia mbaya kutokana na dhambi hiyo na nyingine nyingi.
Hata baada ya dhambi Mungu anamtafuta mtu kwa upendo, ila huyo kwa aibu anamkimbia, au akijisikia analaumiwa na dhamiri, basi anatafuta visingizio hata kumlaumu Mungu kana kwamba ndiye aliyesababisha. Kwa utakatifu wake Mungu hawezi kuvumilia maovu, na kwa haki yake anataka makosa yalipwe. Ndiyo sababu tunakuta matatizo maishani, kama vile uchungu wa uzazi, kuhusiana kwa mabavu, kupata riziki kwa shida, na hasa kufa: hayo yote ni matokeo ya dhambi.
Pamoja na hayo Mungu hapendi mtu yeyote apotee (2Pet 3:9), hivyo toka mwanzo aliahidi kwamba mzawa wa Eva atamponda kichwa shetani (Mwa 3:15). Ndiyo habari njema ya awali kuhusu wokovu ujao.

Maendeleo ya dhambi

Baada ya dhambi ya asili watu walianza kuzaa. Mwa 4:1-16 inatuchorea picha ya Kaini na Abeli kama wazaliwa wa kwanza waliotofautiana kiadili (1Yoh 3:11-12). Toka mwanzo mwovu na mwadilifu waliishi pamoja, wa kwanza akimdhulumu wa pili hata kumuua bila ya kujali udugu. Ikisikitishwa kufikiria mzaliwa wa kwanza kuwa muuaji wa mdogo wake, inafurahisha kwamba wa kwanza kufa alikuwa mwema, kielelezo cha Yesu aliyeuawa bila ya kosa (Eb 12:24).
Toka mwanzo hao walimuabudu Mungu kwa njia ya dini, ibada na sadaka mbalimbali. Hata hivyo Mungu akakubali zile tu zilizotolewa kwa ukarimu (Eb 11:4). Tangu hapo Biblia inatuonyesha jinsi alivyopendelea wadogo kuliko wakubwa.
Kuhusu Kaini tunaonyeshwa ustawi wa dhambi ndani mwake na uongozi wa Mungu aliyemtaka ashinde dhambi bado mlangoni. Hata baada ya dhambi hiyo ambayo ni kubwa kiasi cha kumlilia Mungu alipe kisasi, yeye alizidi kumhifadhi Kaini.
Baadaye (Mwa 4:17-24) kukawa na maendeleo ya aina mbalimbali: ujenzi, ufundi, muziki, lakini hasa dhambi. Picha yake ni Lameki, mtu wa kwanza kuwa na mitara, mkatili kama nini.
Ingawa hali ilikuwa ya kukatisha tamaa, kwa baraka ya Mungu watu wakazidi kuzaa na kati ya watoto wao wakapatikana waadilifu kama Henoko aliyestahili kutwaliwa na Mungu.
Hata hivyo ongezeko la dhambi likasababisha maisha ya binadamu yafupike (Mwa 6:3) kwa kuwa ni kusogea mbali na Mungu, chemchemi ya uhai.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni