Elimunafsia ni fani ya
elimu jamii
inayolenga kujua nafsi ya binadamu ili kurahisisha ukomavu wake na uhusiano wake na wenzake.
Kujifahamu
Hakuna mtu wa
jana, leo au kesho aliye sawasawa na mwingine: kila mmoja ni wa pekee. Mungu
ametufanya tofauti ili tutimilizane. Kila mmoja anahitaji wengine, na kila
mmoja ni muhimu kwa wenzake. Katika maisha ya jamii kuna sehemu ambayo yeye tu
anaweza kuijaza. Wazo hilo linaweza kumsaidia kijana ambaye ni mwepesi kukata
tamaa na kujitupa. Daima uhai ni
zawadi nzuri kwa mhusika na kwa wenzake wote. Kijana ni zawadi yenye nguvu na
wema hata kwa [[taifa, kiasi kwamba kujali ustawi wa kijana ni kujenga taifa.
Tunataka kujifahamu tulivyoumbwa (mwili, nafsi
na roho, ambavyo vyote vinafungamana ndani mwetu):
1. ili
tuweze kujithamini hasa kwa kuona sisi ni nani mbele ya Mungu;
2. ili
tufahamu mipaka yetu na kuikabili inavyofaa;
3. ili
tufahamu vipawa
tulivyojaliwa tuwashirikishe wenzetu;
4. ili
tubadilike kuwa bora zaidi na kuchangia ustawi
wa jamii;
5. ili
tuhusiane vizuri zaidi na wenzetu;
6. ili
tuweze kujieleza kwa watu fulanifulani na kupata mashauri ya kutufaa.
Kujikubali
Daima ni muhimu
tukubali hali ilivyo, halafu tujitahidi kuifanya bora zaidi. Tusipojikubali
kwanza tutahangaika tu hata kukata tamaa. Wajue wasijue vijana wapokua
wanashindwa kujikubali walivyo. Pengine wanaficha silika zao wasitambulikane na watu, hata wakashindwa kujielewa,
wakapatwa na vilema
vya ukuaji
pia. Ni lazima waache kujifunika uso kwa vinyago
hivyo; badala yake wakabili ukweli
wao, wenye sifa na kasoro.
Hivyo tu watapitia vizuri mabadiliko
ya ujana upande wa mwili, nafsi, jamii, maadili na roho.
Hatimaye watakomaa na kushika nafasi yao maishani.
Kwa kila mtu ni
muhimu kuwa na marafiki; hasa kijana anahitaji kikundi. Lakini hiyo isiwe njia
ya kukwepa nafsi yake mwenyewe wala ya kuficha tabia yake kwa kuzungumza,
kutembea au kutenda namna fulani wanavyofanya wenzake. Kwa hiyo asijifananishe
nao. Kila mtu anakua kwa namna yake, akibadilika kwa kiasi tofauti na muda
tofauti. Ni lazima ajifunze kuyapokea mabadiliko hayo pia yanayomfanya geugeu
sana, hasa msichana
katika mzunguko wake wa kila mwezi: mara anaonekana jasiri au korofi, mara
amejaa wasiwasi.
Kujistawisha
Uhai
unasukuma kiumbe chochote kistawi. Mimea inakua namna yake, wanyama namna yao, na binadamu polepole zaidi kwa kuwa ndiye kiumbe
bora anayehitaji kukomaa pande zake zote. Kulingana na haja
yetu ya kukomaa hivyo, sio tu kufikia umri au kimo
fulani, ndani mwetu zimo nguvu zinazotuhimiza tujilinde ili tuzidi kuishi
wenyewe, tuendeleze uhai tulionao kwa kuzaa, tujitegemee (yaani tumiliki maisha
yetu), tutawale vitu na watu ili mambo yaende tunavyotaka, n.k. Haja iliyoota
mizizi mirefu ndani mwetu ni ile ya kujikamilisha tusiwe watu wanaoishi ili
mradi tu. Kadiri tunavyokua tunajisikia kuwajibika. Haja hizo zinafanya
tujiwekee pia malengo katika utendaji.
Basi, baada ya kujifahamu, kila mmoja wetu achague na kuazimia awe bora vipi,
kwa sababu wenyewe tunaamua tuweje.
Ni wajibu
wetu kujipenda na kwa hiyo kujitunza na kujistawisha kimwili, kinafsi, kijamii,
kimaadili na kiroho. Kazi hiyo inahitaji nia na bidii za kudumu. Tufuate
taratibu za kulinda afya ya mwili,
heshima
ya mavazi, usafi wa mazingira. Tujiepushe na uvivu
unaosababisha mawazo na matendo mabaya. Tujihadhari na maandishi, picha na
maneno yasiyofaa, yasije yakatupotosha kimawazo au kusisimua ashiki.
Tuhusiane vema na wengine (adabu, lugha
nzuri n.k.). Hasa tufuate dhamiri na kustawisha roho
iliyo sehemu bora ya utu wetu
ambamo tunashirikiana na Mungu. Mbali ya motisha
kutoka nje (yaani kupewa tuzo au adhabu),
sisi binadamu tuna maarubu
yanayotuongoza kwa ndani na kututia nguvu tutende namna fulani na kukwepa mambo
mengine. Yanaweza kuwa ya aina mbalimbali:
1. tusiyofundishwa
kwa kuwa ni haja za
mwili (kupumua, kunywa, kula, kujisaidia, kupumzika, kutumia jinsia
n.k.) au haja za
nafsi (kupendwa, kufungamana, kukubaliwa, kufanikiwa, kujitokeza,
kusaidia, kushindana, kushinda, kutawala, kujihami, kuwa salama, kuongozwa,
kujishusha, kujitawala, kumiliki, kupanga, kubadili, kujua, kuhemka,
kujamiiana, kucheza);