Mtayarishaji

Morning Star Radio

Alhamisi, Januari 06, 2011

KUPANDA KWA HALI JOTO DUNIANI

Kupanda kwa halijoto duniani kunaonekana kwa kulinganisha vipimo vya halijoto vinavyopatikana. Kupanda huku kunaleta mabadiliko ya hali ya hewa yaliyoanza tayari kuathiri maisha ya watu na uhai duniani kwa ujumla.

Kuna hofu ya kwamba mabadiliko haya yataleta hatari kubwa kwa jamii za watu.

Kati ya wanasayansi kuna tofauti ya maoni kama sababu za mabadiliko ni shughuli za kibinadamu au kama kuna sabau asilia. Siku hizi wataalamu wengi wanafikiri ya kwamba sababu kuu ni kuchoma kwa makaa na mafuta katika viwanda, magari na vituo vya umeme kunachopuliza gesi hewani kama dioksidi kabonia.


Vipimo na data

Duniani kuna upimaji wa kisayansi wa halijoto tangu mwaka 1860. Kabla ya hayo kuna kumbukumbu ya hali ya hewa katika karne zilizopita kutoka mahali mbalimbali ambazo hazikusanifishwa wakati ule. Leo hii wanasayansi wanatumia vipimo na taarifa za kale wakipiga makadirio juu ya hali ya hewa katika historia.

Hapo wanatumia pia mbinu kama kulinganisha miviringo kwenye mashina ya miti inayonyesha miaka yenye mvua mwingi au kidogo au wanapima kiwango cha dioksidi kabonia kwenye barafu ya chini nchani yenye umri wa miaka 10,000 na zaidi.

Kwa jumla makadirio ya hali ya hewa hutofautiana lakini kwa jumla kuna picha juu ya miaka 1,000 iliyopita. Watalaamu wanakubaliana ya kwamba mnamo mwaka 1000 kulikuwa na kipindi cha joto kiasi na tena kipindi cha baridi kiasi kuanzia manmo mwaka 1600.

Lakini hakuna uhakika bado juu ya athira duniani kwa sababu sehemu kubwa ya data ni kutoka upande wa kaskazini ya dunia.

Vipimo vya kisayansi vinavyopatikana vinaonyesha ya kwamba halijoto ya wastani duniani imepanda sentigredi 0.7 kati ya 1906 na 2005. Hii si kiwango kidogo; wakati wa zama za barafu kubwa miaka 100,000 iliyopita halijoto ilikuwa tu 6 °C chini ya wastani ya leo na hii ilitosha kufunika seehmu kubwa za Ulaya, Asia na Amerika ya Kaskazini na mabapa manene ya barafu.

Dalili zote zinadokeza ya kwamba kupanda kwa halijoto kuliharakishwa tangu 1970 na kunaelekea kupanda zaidi.


Sababu za kuongezeka kwa halijoto

Kwa miaka kadhaa wataalamu hawakukubaliana juu ya sababu za kongezeka kwa halijoto. Kwa jumla kuna maelezo mawili tofauti:

  • Kupanda kwa halijoto ni jambo la kawaida lenye sababu asilia; historia inaonyesha vipindi vya joto na vipindi vya baridi na sababu kuu ni mabadiliko ya kiwango cha mnururisho wa jua uanofika duniani. Mabadiliko haya hayakueleweka bado lakini labda kuna kitu kama majira ya jua yenyewe yanaobadilia kila baada ya miaka mia kadhaa.
  • Kupanda wa halijoto kwa sasa si jambo la kawaida kwa sababu kunaenda sambamba na kuongezeka kwa gesi kama dioksidi kabonia hewani kutokana na shughuli za kibinadamu hasa kuchoma kwa makaa na mafuta ya petroli.

Siku hizi wataalamu wengi wanelekea upande wa pili maana wanaona mbali na sababu asilia kuna athira za kibinadamu zinazobadilisha hali ya hewa.


Matokeo yanayotarajiwa

Wataalamu wanaonya ya kwamba kupanda kwa halijoto inaweza kuleta mabadiliko kama yafuatayo:

  • kuongezeka kwa halijoto ya angahewa itaongeza pia halijoto ya bahari na kusababisha uvukizaji mkubwa utakaoleta mawingu na mvua wa nyongeza duniani
  • mikondo ya bahari itabadilika na kubadilisha hali ya hewa katika nchi nyingi
  • sehemu kadhaa penye jangwa zitapokea mvua lakini maeneo mengine yatakosa mvua hivyo kuleta matatizo kwa kilimo na njaa kwa watu
  • barafu kwenye ncha za dunia itaendelea kuyeyuka. Hii itasababisha kupanda kwa uwiano wa bahari, kuleta mafuriko kwenye pwani za dunia na kuhatarisha makazi ya watu karibu na bahari hasa miji ya bandari na nchi za visiwani. Nchi kadhaa kama Maldivi zitazama baharini na kupotea kabisa.
  • Kwa jumla upepo na tufani zitaongezeka na kuwa kali zaidi
  • Magonjwa kama malaria yataongezeka kwa sababu mbu wanaopitisha ugonjwa watapata nafasi mpya katika sehemu zilizokuwa baridi mno hadi sasa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni