Mtayarishaji

Morning Star Radio

Jumatatu, Januari 17, 2011

DHAHABU ISIYOOZA..!!

Kwa takribani miaka mitano iliyopita tuliupigia debe kihalali mtindo mpya wa muziki wa A cappella katika radio ya injili Morning Star 105.3 fm-Dar es salaam, ni mtindo unaojichanganya vema ndani ya mitindo kadhaa.

Mtindo huu kwa sasa umewateka watu wengi hapa nchini na hata duniani kote, hivyo kujitambua kwetu kwa mada hiyo miaka iliyopita kumeibua mwamko wko mdau. Nilipokea maoni kadhaa kutoka kwa wadau mbalimbali waliowasiliana nami, kuna waliotoa changamoto kwamba tufanye matamasha makubwa yatakayoupa kipaumbele muziki wenye vionjo hasa vyetu. Ukatolewa mfano wa nchini Jamaica, ambako hufanyika matamasha makubwa ya reggae na ragga kila mwaka.

Hayo yalikuwa maoni kutoka kwa msikilizaji wa kipindi cha Muziki wa Acappela ambacho hurushwa kila ijumaa kuanzia saa 2:00-3:00 usiku 105.3 fm-Dsm, lakini niliguswa zaidi na maoni ya mdau mwenzangu wa muziki kwa upande wa habari. ambaye ni mwandishi nguli wa taarifa za kimuziki za kimataifa hapa nchini, alinipa changamoto njema niliyoifanyia kazi na kupata si haya unayoyasoma tu. Kwa muktadha huo basi, leo tunaendeleza tena libeneke la Acappella kwenye safu yetu japo sasa sio radioni.

Aliniuliza swali: “Vipi unawafahamu Black Mambazo, wanamuziki wa miondoko ya Acappela kutoka Afrika ya Kusini?” nilimjibu kuwa ninafahamu vyema sana.

Akasema kuwa mara kadhaa amewashuhudia kwenye video zao hasa za jukwaani, akaniuliza: “Mbona wanaimba na kucheza baadhi ya nyimbo zao kama hii miziki ya asili iliyopo hapa Tanzania? au sisi tumeiga kutoka huko?”

Kwa kifupi nilimjibu kuwa hii Acappella tunayoifahamu, ni moja kati ya awamu ya mtindo mmoja katika maeneo mengi. Lakini kina cha majibu hayo kwa mjadala ulioendelea baina yangu na Mdau, ni kukupatia ufahamu zaidi wa dhahabu isiyooza ambayo sasa tunaweza kuipangusa ili iendelee kung’ara sio tu iwe kama zamani!! zaidi ya zama hizo.

Kwa mujibu wa utafiti Acappela ni moja ya mitindo ya kale kabisa ya Kiafrika, ulioanzia miongoni mwa jamii za Kibantu zenye utajiri mkubwa sana wa mitindo mbalimbali ya kucheza ngoma zenye maudhui mbalimbali.

Kwa hiyo ukisema ya kale ni dhahabu maana yake ni kwamba, inawezekana kabisa kuwa watoto wadogo wa mitaa ya Uswahilini hapa nchini walinogewa kuimba mtindo huo kwa kuuona kutoka mahali fulani huko nje.

Si lazima wafike huko ili waone, maana kiteknolojia video na audio za muziki zipo na huonyeshwa hata katika vituo vya runinga na kuchezwa radioni. Ushahidi wa dhahabu isiyooza ni Afrika, kuucheza mtindo huo ambao kwa kizazi hicho cha watumwa waliochukuliwa ughaibuni si kitu cha ajabu. Jasiri haachi asili na hiyo maana yake ni kuwa kizazi cheusi ughaibuni kimeendelea kubeba thamani kubwa ya utamaduni wake.

Hizo ndizo chembe chembe zilizoingia katika mitindo mingi ya kimataifa, ambayo wengi msiyoifahamu vyema mnadhani ni ya kigeni kabisa kwetu Waafrika. Nikutajie baadhi ya mitindo yenye vionjo hivyo, kuna r ‘n’ b, reggae, blues, ballads na hip-hop.

Nitakulinganishia asili yake ili ujue vionjo vya Kiafrika ndani yake, r ‘n’ b (rhythm and blues) ni ‘mkong’osio’ na ‘simanzi’ muziki wa maombolezo ya madhila ya utumwa.

Reggae ni muziki uliotokana na ibada za jadi za Kiafrika kupitia dini ya Kiafrika ya Urastafari, blues ni muziki unaopigwa na Wanubi au zeze unaozungumzia huzuni na huko ughaibuni hupigwa zaidi kwa gitaa moja.

Ballads ni nyimbo za taratibu za simulizi za mapenzi, kama ngoma za kumsifia binti aliyejitunza hadi wakati wa kuolewa. Hip-hop (rap) ni ngonjera za majigambo, kama ilivyokuwa kwa ghani za kina hayati Mwinamila.

Kwa mashiko ya Waafrika kimuziki huko ughaibuni, ndiyo maana ni kizazi cheusi ambacho kwa sehemu kubwa kinatamba kimuziki duniani.

Hata Michael Jackson ana nyimbo nyingi ambazo ukitazama uchezaji wake wa vyombo, kuna ngoma za kienyeji za maeneo ya Afrika Magharibi. Hii ndiyo dhahabu isiyooza ambayo pia imo ndani ya Acappella ambayo tukiing’arisha vyema itakuwa rahisi kutufanya tung’are kimataifa.

Kama dhahabu hii tutaitumia vyema basi ni rahisi kujikubalisha, kama ambavyo Wakongo walivyopokea bila kujua muziki ambao ulianzia kwao ukaenda kimataifa. Lakini uliporudi tena wakaukumbatia na kuutia unguli wa vionjo vipya, ndipo ikapatikana mitindo yao ya mabolingo.

Ndiyo maana mijadala ya miaka iliyopita juu ya namna gani tutapata mtindo wetu wa muziki kimataifa Tanzania, kwa majaribio kama ya maabara kwa kujilinganisha na Wakongo ikakosa mashiko na kutofanikiwa.

Tusingeweza kushindana na mitindo yenye mizizi mirefu ya miaka mingi, kwa kuwa tulitaka kutumia njia tofauti lakini kwa bahati njia muafaka imejileta yenyewe kupitia Acappella.

Hii maana yake ni kwamba tuna dhahabu ya Acappella yenye vumbi, ambayo tunapaswa kuipangusa ili itung’arishe. Wasani/Waimbaji kama tumeshaligundua hilo hatuna budi kulifanyia kazi, naamini tutafanikiwa kupata alama yetu ya kitaifa kimuziki iliyotupiga chenga kwa miaka mingi mno.

Bwana ni hivi, kwanza Sanaa mbele!Na ndio maana kinachofuatia sasa kuanzia 2011 ni ACAPPELLA MTAANI.


Maoni 4 :

  1. Nakuaminia mkuu, `ya kale ni dhahabu, lakini hiyo dhahabu kama imefichwa shimoni, itakuwa na thamani sawa na ile iliyopo benki...sijui nilikuwa nawaza tu mkuu!

    JibuFuta
  2. ACAPPELLA poa!

    Na inasemekana ndio asili ya uimbaji kabla hata BINADABU hajastukia kuwa sauti inahitaji kusaidiwa na vyombo kama ngoma , MAGITAA , piano au tu makopo yagongwegonwe ndio kieleweke!

    JibuFuta
  3. Ni kweli mkuu nashukuru kwa hekima hii adimu, kama dhahabu yenyewe, lakini ile isiyo-oza

    JibuFuta
  4. Great article. Inafunza mengi na ni busara kwa wengi kusoma (japo si jadi yetu).
    Pengine wanaojishughulisha na kuielimisha jamii kupitia radio wanastahili kujua wanalotaka kufanya na hata muziki wanaotaka kuwasikilizisha wasikilizaji wao kwani "there is a story behind every music"
    Blessings

    JibuFuta