Mara nyingi wazungumzaji wa methali za Kiswahili huanza kwa kusema ‘wahenga
walisema....’ au ‘kama wahenga walivyosema....’
huwa zinaitwa methali kutokana na umri wake katika jamii ina "ukweli" kiasi gani? Je,
vijana hawawezi kuwa na methali zao? Je methali hutokeaje? Na je, ili usemi uweze
kuitwa methali hauna budi uwe na umri gani katika jamii? Maswali haya nilijiuliza baada
ya mjadala kwamba UKIMWI haujakaa katika jamii kwa muda mrefu wa kutosha
kuweza kuzua methali.
Suala la methali hutokeaje, na umri gani uwe wa kutosha limeangaliwa na akina
Omari, Kezilahabi na Kamera (1975). Wao wanasema kwamba misemo ikikaa kwa muda
wa kutosha katika jamii, hata kuwa na kufanana toka jamii moja hadi nyingine, ikisema
kwa kifupi "busara" za wahenga, basi hubadilika kuwa methali. Je umri wa kutosha ni
upi? Tunaikubali fikra kwamba ili usemi uitwe methali hauna budi kuwa umeenea katika
jamii mbalimbali.
Jambo muhimu la kujadiliana ni kuhusu misemo na methali. Je ni wakati gani
msemo hukoma kuwa msemo na kuanza kuwa methali? Bila shaka mojawapo ya sifa
zitakikanazo ni msemo kuwa umeenea mahali pengi. Uwe unafanana katika jamii nyingi.
Hiki ni kigezo cha msingi. Hata hivyo, ikumbukwe kuwa namna za kueneza usemi kama
huo leo ni tofauti kabisa na jinsi ilivyokuwa miaka ishirini na mitano iliyopita. Ni tofauti
na jinsi ilivyokuwa miaka hamsini iliyopita. Leo hii kutokana na mapinduzi katika
mifumo ya mawasiliano, jambo linaweza kusemwa sehemu moja na likasikika sehemu
nyingi kwa wakati mmoja na kwa upesi sana. Leo hii, radio na televisheni zinarusha
matangazo dunia nzima katika jamii nyingi na kwa lugha mbalimbali kwa kasi ya hali ya
juu.
Uwezo huu wa teknolojia unalazimisha mabadiliko katika nadharia mbalimbali
zilizokuwapo hapo awali. Hii leo usemi mmoja unaweza kuenezwa kwa njia mbalimbali
kwa haraka na kwa mvuto tofauti. Kwa mfano matangazo ya biashara katika televisheni
yanavutia zaidi leo na yanaweza kuenezwa kwa haraka zaidi kuliko ilivyokuwa hapo
mwanzo. Uanzishwaji wa matumizi ya simu za mikononi umeleta mapinduzi makubwa
katika mawasiliano. Leo hii usemi mfupi uliobeba muhtasari wa mawazo fulani ya jamii,
unaweza kuenezwa kwa siku moja na ukaanza kutumika haraka miongoni mwa vijana,
watu wazima au watoto kwa kadri utakavyokuwa umewekwa. Kwa mtindo huu huu, leo
hii matangazo kuhusu UKIMWI yanarushwa kwa haraka, yanawafikia watu wengi zaidi
na kwa njia mbalimbali.
Tukiangalia hali ya teknolojia Tanzania na wakati wa UKIMWI, tunaona kuwa janga
hili "limezushwa" duniani si zaidi ya miaka thelathini iliyopita. Huu ni wakati ambapo
nchini Tanzania kulikuwa na mabadiliko makubwa katika teknolojia ya habari na
mawasiliano. Zilianzishwa redio kadhaa, na nchi ikapata televisheni zaidi ya moja.
Mabango ya matangazo yalianza kujaa barabarani na simu za mikononi zilianza kuenea
nchini. Njia hizi zote ziliwezesha kuanzishwa kwa misemo na semi mpya na kuzieneza
kwa haraka katika jamii za Waswahili, Afrika ya Mashariki. Aidha, baadhi ya semi na
misemo mingine iliyokuwapo ilibadilishwa na kuenea kwa haraka hasa miongoni mwa
vijana.
Katika mtazamo huo basi tunaweza kusema makala haya yanatoa changamoto
kubwa katika kuangaliwa upya kwa utanzu wa fasihi na uhusiano uliopo kati ya utanzu
huo na mabadiliko katika teknolojia ya habari na mawasiliano. Ni jambo la kuzingatia
kwamba yafaa maana za tanzu mbalimbali za fasihi ziendane na jamii iliyopo, na wakati
huo huo ziwe na sifa za kukivuka kizingiti cha wakati.
Umuhimu mwingine wa makala haya ni kuchochea udadisi mpana zaidi katika
tanzu za fasihi. Ni matarajio yangu kuwa msomaji atataka kujua hasa maana ya leo ya
methali ni nini. Mwingine baada ya kusoma makala haya anaweza kusema, 'utanzu
mmoja wa methali hautoshi kuonesha athari za UKIMWI katika tanzu za fasihi', hivyo
akatafiti na kuandika kuhusu athari za UKIMWI katika tanzu nyingine mbili au tatu.
Ikitokea hivyo, makala haya yatakuwa yamefanikiwa kuchochea udadisi sio tu wa ni nini
maana ya methali, bali pia athari ya UKIMWI katika tanzu nyinginezo za fasihi.
Labda nihitimishe sehemu hii kwa kusema kuwa kuendelea kutumiwa kwa misemo
hiyo na wanajamii, hasa misemo inayohusu UKIMWI, kunanifanya nijiulize swali moja
ambalo ndilo linalonishughulisha katika makala haya. Ninataka kujua athari za UKIMWI
katika tanzu za fasihi. Nitafanya hivyo kwa kuitazama athari hiyo katika utanzu wa
methali kwa kutumia dhana ya ambayo nimeamua kuiita