TUNASAFIRI kwa ndege katikati ya
mawingu mazito na hivyo hatuwezi kuona chochote. Kwa ghafula, ndege yetu
inatoka kwenye mawingu na chini yetu tunaona eneo la Aktiki
lililofunikwa kwa theluji. Mandhari hiyo inapendeza kama nini!
Tunapotazama mabamba ya barafu, mikono ya bahari, na milima iliyofunikwa
kwa theluji, tunastaajabu. Ni kana kwamba eneo hilo lisilo na mimea
lililofunikwa kwa theluji na barafu halina mwisho. Tumekuja kutembelea
Svalbard, visiwa vilivyo karibu na Ncha ya Kaskazini, kati ya digrii 74
za latitudo na digrii 81 kuelekea kaskazini!
Jina Svalbard, linalomaanisha “Pwani
Baridi,” lilionekana kwa mara ya kwanza mnamo 1194 katika maandishi ya
Waiceland. Lakini eneo hilo “liligunduliwa” miaka 400 baadaye, mnamo
1596 na hivyo likajulikana ulimwenguni pote. Mwaka huo kikundi cha
wagunduzi Waholanzi kikiongozwa na Willem Barents kilikuwa kikisafiri
kwa meli kuelekea kaskazini wakati ambapo mmoja kati yao aliona kwenye
upeo wa macho yake eneo lisilojulikana, safu ya milima yenye ncha.
Wagunduzi hao walikuwa kwenye eneo la kaskazini-magharibi mwa Svalbard,
naye Barents aliita eneo hilo “Spitsbergen” jina linalomaanisha “Milima
Iliyochongoka.” Hilo ndilo jina la kisiwa kikubwa zaidi kati ya visiwa
hivyo. Ugunduzi wa Barents ulianzisha kipindi chenye utendaji mwingi
huko Svalbard. Utendaji huo ulitia ndani kuvua nyangumi, sili,
kuwakamata wanyama, kugundua maeneo mapya, kuchimba makaa ya mawe,
kufanya utafiti wa kisayansi, na utalii. Kwa miaka mingi, nchi kadhaa
zimeshiriki katika utendaji huo, lakini kuanzia mwaka wa 1925 visiwa
hivyo vimekuwa chini ya utawala wa Norway.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni