Ndani ya bahari
samaki-gamba mkubwa sana anasonga polepole kati ya miamba, akila
magugu-maji yanayoyumbishwa na mikondo ya bahari. Gamba lake la nje
lililofunikwa kwa asidi na viumbe vidogo vya maji, hufanya isiwe rahisi
kuona rangi zake nyangavu, yaani, rangi tofauti-tofauti za bluu, kijani,
na zambarau zilizochangamana na manjano na waridi, na sehemu ndogo
zilizo na rangi ya dhahabu na fedha.
Kiumbe huyo wa kushangaza ni paua,
wa jamii ya moluska anayepatikana New Zealand peke yake. Kiumbe huyo na
viumbe wengine wa jamii hiyo wanaishi chini ya maji karibu na pwani
zenye miamba. Ingawa paua anapendwa kwa sababu ya rangi za
kupendeza za gamba lake la ndani linaloweza kutumiwa kutengeneza vito
maridadi, watu wengi wanapenda nyama yake tamu. Kwa kuongezea, lulu
zenye kung’aa sana zinaweza kukuzwa ndani yake.
Kuna jamii zaidi ya 100 za
moluska ulimwenguni pote zinazopatikana Afrika Kusini, California huko
Marekani, Japani, Australia, na katika kisiwa cha Guernsey kilicho
kwenye Mlango-Bahari wa Uingereza. Hata hivyo, katika eneo la kusini la
bahari ya Pasifiki Kusini ndiko tu unaweza kupata moluska mwenye rangi
nyangavu wa New Zealand, anayeitwa paua (Haliotis iris).
Muujiza wa Kibiolojia
Ndani ya gamba la paua, matabaka ya protini na kalisi hukusanyika na kutokeza rangi maridadi kama jiwe la thamani linaloitwa opali. Kwa sababu hiyo, paua
amejulikana kuwa jiwe hilo la thamani la baharini. Kiwango cha joto
baharini kinaposhuka, moluska hulala. Kisha matabaka ya magamba yao
huchukua muda mrefu zaidi kukua. Mtaalamu mmoja anaamini kwamba rangi
mbalimbali za paua huenda zinatokana na virutubisho katika maji na pia rangi mbalimbali za magugu-maji ambayo moluska hula.
Paua huchagua chakula chao
kwa uangalifu na vilevile wao huchagua wataishi karibu na nani.
Hawawezi kuishi karibu na mwanamizi mwenye miiba, au kina, kwa
sababu wanakula aina zilezile za magugu-maji. Pia, kiti cha pweza ni
adui hatari kwani wachache tu kati yao wanaweza kumaliza familia nzima
ya paua. Kwa ujanja, kiti cha pweza huwekelea mnyiri kwenye mashimo ya kupumulia ya paua na hivyo kufanya asiweze kupumua. Kisha, paua anapoanguka kutoka kwenye jiwe alilolalia, kiti cha pweza humla kwa urahisi.
Matumizi Mbalimbali ya Paua
Ingawa sehemu nyeusi ya nje ya paua haipendezi sana, kwa karne nyingi wenyeji wa New Zealand wanaoitwa Wamaori wamekula paua. Sehemu inayoweza kuliwa ya paua
ni musuli mkubwa, au mguu, ambao kiumbe huyo hutumia kusonga kwenye
miamba. Pia Wamaori wametumia gamba lake katika mapambo na kama chambo
cha kuvua samaki. Wametengeneza vito kwa kutumia magamba yake na
wameyatumia kama macho katika michongo yao.
Sasa paua anapendwa sana kuliko wakati mwingine wowote. Watalii hawakosi kununua vito vya paua wanapotembelea New Zealand.
Leo, watu wanaopiga mbizi bila vifaa vya kupumua, wanawavua paua
kwa wingi sana. Hiyo imekuwa biashara inayoletea New Zealand dola
milioni nyingi sana kutoka kwa nchi za nje. Ili kuhakikisha kwamba paua hawaangamizwi huko New Zealand, serikali imeweka kiwango cha paua
wanaoweza kuvuliwa kwa mwaka. Nyama nyingi hutiwa katika mikebe ili
ikauzwe huko Asia, na nyingine hugandishwa na kutumwa Singapore na Hong
Kong ambako paua wanapendwa sana ingawa wanauzwa kwa bei ghali sana. Mara nyingi, analiwa akiwa mbichi na kukatwa vipande-vipande. Ingawa kuna paua wengi sana huko New Zealand, wenyeji wengi hawajawahi kuonja nyama yake kwa sababu ya kuuzwa sana katika nchi za nje.
Ili waweze kutosheleza uhitaji wa kimataifa wa paua,
wafanyabiashara wanatumia mbinu za kisasa kuwafuga. Wafanyabiashara
huko Australia, Japani, na Marekani wamefaulu kutumia mbinu hiyo ili
kufuga moluska wengine. Mbinu mpya kama hizo zimesaidia paua wafugwe katika matangi yenye mifumo ya kudumisha kiwango kinachofaa cha joto mbali sana na maeneo wanayopatikana kwa ukawaida.
Paua wa kufugwa wanakula
kwa kiasi kilekile kama wale wa kiasili. Kila juma wanaweza kula chakula
chenye uzito sawa na nusu ya uzito wao. Kwa kushangaza, paua pia wanaweza kusonga haraka. Wanapopinduliwa, wanaweza kujigeuza upesi sana. Ni kazi rahisi kufuga paua. Mtaalamu mmoja anasema kwamba “inafurahisha kufuga paua kwa sababu ni wapole na wenye adabu, na hawawasumbui wafugaji!”
Lulu za Paua
Zaidi ya kutokeza vito vinavyotengenezwa kutokana na magamba yao na kutumiwa kama chakula, paua wanaweza pia kutokeza lulu zenye kung’aa. Ni vigumu kupata lulu za asili katika paua
wanaoishi baharini. Lakini wanaweza kutokezwa kupitia mbinu iliyobuniwa
katika miaka ya 1890 na mwanasayansi Mfaransa Louis Boutan. Kito chenye
umbo la yai kilicho na rangi za kuvutia kama za gamba la paua hutokezwa. Mbinu hiyo hufanya kazi jinsi gani?
Vipande vya udongo, mbao, mfupa, au chuma, huwekwa ndani ya gamba la paua katika sehemu tatu, yaani, mara mbili kwenye upande na mara moja mgongoni. Pole kwa pole, paua hufunika vipande hivyo vilivyoingizwa ndani ya gamba lake kwa matabaka ya lulumizi, yaliyotengenezwa kwa kalisi kaboni, na conchiolin.
Kwa angalau miezi 18, maelfu ya matabaka hutokezwa na kufanyiza lulu
ndogo. (Ona sanduku lililo chini.) Inachukua miaka sita ili kufanyiza
lulu kubwa. paua 1 hivi kati ya 50 hutokeza lulu ambayo
imekaribia kuwa kamili. Hii ni lulu laini, yenye rangi nyangavu, na
inayong’aa kwa kustaajabisha.
Bado watafiti hawajafaulu kutokeza lulu yenye umbo la mviringo kutoka kwa paua. Hiyo ni kwa sababu, tofauti na chaza, paua
ana musuli katika tumbo ambao hutema kitu chochote kinachowekwa katika
mfumo wake wa kumeng’enya. Huenda siku moja mtu akagundua siri ya
kutokeza lulu ya mviringo.
Kwa sasa, tunaweza kufurahia
vitu tunavyopata kutoka kwa samaki-gamba huyu aliye na matumizi mengi,
yaani, vito vyenye kupendeza, nyama tamu, na gamba lenye rangi maridadi.
Je, hatumshukuru Mungu kwa kutupa zawadi yenye kupendeza kama hiyo?—Yakobo 1:17.