Mtayarishaji

Morning Star Radio

Alhamisi, Septemba 13, 2012

Lugha ya adabu yafifia Kenya



Lugha ya adabu ni lugha wanayotumia wazungumzaji ambayo huficha makali ya baadhi ya maneno wanapoyatamka. Inawezekana pia kusema ni lugha ya heshima. Ni muhimu kujua pia lugha hiyo huambatana na mafumbo ama semi. Katika fasihi inaitwa tasfida. Kenya kufikia sasa kuna ukame wa msamiati wa adabu. Mathalan majina kama tafadhali, naomba, samahani, niwie radhi na kadhalika yanasikika sana katika vinywa vya Watanzania wakiwasiliana japo kwa wakenya sivyo.

Hata hivyo zipo sababu nyingi zilizochangia hali hiyo kuwa ilivyo. Mwanzo upo mmomonyoko wa maadili miongoni mwa wakenya. Yaani baadhi ya wazungumzaji Kenya hawaoni sababu ya kusema kwa mfano 'haja kubwa' badala ya kutaja neno hilo moja kwa moja. Wengine hawataki kujitaabisha kujipinda huku na kule. Wanaamua kutaja neno hilo moja kwa moja. Ukiwauliza watakwambia kuwa si makosa wakisema mwanamke ana mimba badala ya kusema ni mja mzito.

Aidha mazingira huchangia pakubwa hulka ya watu katika masuala haya ya lugha ya adabu. Kwa mfano nchini Kenya sehemu za pwani kuna idadi kubwa ya watu wanaozungumza lugha ya adabu. Ni huko ndio utapata salamu za shikamoo na majibu ya marahaba kwa wingi. Pengine ni kwa sababu kuwa baadhi yao hawana haraka na hata wanapokutana na mtu wanataka kumjulia hali kikamilifu.Ni huko huko utasikia mara nyingi watu wakisema Fulani ameaga dunia bali si yule mtu amekufa. Katika sehemu hizo utamsikia mtu akisema naenda kutema mate badala ya kusema naenda kukojoa.

Si hayo tu, tofauti za watu kisiasa, kijamii na kiuchumi zina mchango mkubwa katika matumizi ya lugha ya adabu. Kwa mfano mhadhiri wa chuo kikuu nchini Kenya atapata shida sana ya kujitafadhalisha mbele ya mwanafunzi wake. Mara nyingi ni mwanafunzi anayenyenyekea mbele ya mwalimu. Katika bunge la Kenya kwa mfano wabunge ndio watakaolazimika kutumia majina kama mheshimiwa spika wakichangia mijadala bungeni. Ni vigumu spika kujitafadhalisha anapotoa uamuzi. Kwa ufupi idadi kubwa ya wakenya ni waasi wa lugha ya adabu. 

Source: Bbc Swahili - Na Paul Nabiswa.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni