Mtayarishaji

Morning Star Radio

Jumatano, Julai 11, 2012

ISHARA YA KUTAMBUA

Picha kwa hisani ya: www.telecomcircle.com

MASWALI yanaibuka. Je, kikosi kilichomteka daktari huyo na kumpeleka kwenye msitu wa Mabwepande, Dar es Salaam kimefadhiliwa na serikali au magaidi?
Dokta Steven Ulimboka, mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari alikumbana na kikosi cha watekaji, watesajii na wauaji. Kama ni magaidi walikusudia nini? Magaidi walikuwa na nongwa ipi na Dk. Ulimboka? Watekaji wametoa ujumbe wowote? Je, kuna historia ya ugaidi wa namna hii nchini?

Je, watekaji hawawezi kuwa mawakala wa serikali? Je, hakiwezi kuwa kikosi maalum cha kutesa watu kwa siri chini ya udhamini wa serikali? Jibu la maswali mawili hayo ni ndiyo, maana hiyo, ndiyo hasa ina nongwa na Dk. Ulimboka aliyeongoza mgomo wa madaktari nchi nzima kudai hali nzuri ya utumishi.

Sikia. Mtu wanayemfahamu kutoka ikulu anampigia simu Dk. Ulimboka ili wakutane kujadili ufumbuzi wa mgomo. Dk. Ulimboka na mwenzake Dk. Deogratius Michael wanakwenda eneo la kikao; wanamkuta mtu anayejiita Abeid; lakini ghafla wanatokea watu na kumchukua yeye tu.

Watekaji wanakwenda naye Mabwepande, msitu uleule ambao mwaka 2006, polisi wa serikali walitumia kuua watu wanne – wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge, Morogoro na dereva teksi mmoja.

Vijana wale wafanyabiashara walitekwa na polisi, wakateswa, wakaporwa mali waliyokuwa nayo kisha wakatwangwa risasi za kisogoni – wakafa. Unyama mkubwa. Mambo yalipojulikana, polisi wakadai kuwa walikuwa majambazi.

Rais Jakaya Kikwete akaunda tume; ikahoji watu, ikapata ushahidi kwamba polisi walihusika kuteka, kuwapeleka msituni na kuua. Kesi ikafunguliwa, lakini “mahakama” ikasema polisi walioteka na kuwapeleka Mabwepande na kuua hawana hatia; ikawaachia!

Wiki iliyopita, ‘mawakala’ waliokuwa na nongwa kubwa na mgomo, wakafanya juhudi usiku wa kuamkia siku ambayo serikali ilisema itatoa msimamo juu ya mgomo huo, wakatekeleza lile Waziri Mkuu, Mizengo Peter Pinda alilosema “…liwalo na liwe” wakamteka, wakampiga, wakamng’oa meno na kucha kushinikiza ametumwa na nani kuongoza mgomo. Serikali inatoka vipi hapa?

Mwaka 2008 Pinda alisema wanaoua albino wauawe, kauli inayotafsiriwa sasa kuwa hata wanaoua watu kwa njia ya mgomo wauawe. Ndiyo, waliotenda unyama huo wakawapigia simu madaktari wakachukue “mzoga” wao.

Serikali imekana kuhusika. Lakini hakuna serikali yoyote duniani iliyowahi kukiri kuhusika katika mauaji ya wanasiasa au wanaharakati au waandishi wa habari au wapinzani.

Vikosi maalum vya kuteka watu, kuwapoteza, kutesa na hata kuua, hutekeleza unyama huo kutetea au kulinda maslahi fulani, kama vile biashara haramu au ufisadi au maslahi ya kisiasa.

Mathalani magenge ya wahuni na wauzaji wa dawa za kulevya Mexico na Colombia huteka viongozi wa juu serikalini au jamaa zao na hushinikiza walipwe mamilioni ya dola kama kikombozi.

Magaidi wa Colombia waliounda jeshi linalofahamika kama Revolutionary Armed Forces of Colombia (FARC) huteka, hutesa na kuua viongozi wa serikali wanaopinga biashara ya dawa za kulevya.

Miaka ya 1970 vilikuwepo vikundi vingi vya kigaidi na kimojawapo kiliongozwa na Ilich Ramírez Sánchez “Carlos the Jackal,” raia wa Venezuela.

Matukio ya kuteka na kuua wanasiasa yakifanywa na vikundi vya watu, serikali hutumia rasilimali zake zote kuwasaka wahusika.

Hii ndiyo sababu, Carlos ambaye aliitesa sana Ufaransa na kuvamia ofisi za makao makuu ya Umoja wa Nchi za OPEC mjini Vienna, Austria mwaka 1975 na kuua mawaziri watatu na wengine 63 kutekwa wakiwemo mawaziri 11, alinaswa na sasa anatumikia kifungo cha maisha jela nchini Ufaransa.

Hata Osama bin Laden aliyetikisa dunia kuanzia miaka ya 2000, aliuawa huku kikundi cha Al-Shaabab cha Somalia kikisakwa. Ikumbukwe kila kikosi cha watu maalum kikiteka watu maarufu, hulenga ama kulipwa fedha au kushinikiza wenzao waliofungwa waachiwe kabla hawajauawa au masuala ya siasa.

Lakini huwa vigumu kuikamata serikali. Ukweli hata kama serikali itakanusha, kama ilivyofanya sasa kwa Dk. Ulimboka au kwa mkurugenzi mstaafu wa Usalama wa Taifa, Imran Kombe na kwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Zanzibar, Abdullah Kassim Hanga na wengineo, ushahidi wa mazingira unathibitisha serikali inahusika.

Katikati ya mapambano dhidi ya ufisadi, Mkurugenzi wa MwanaHALISI, Saed Kubenea alipigwa ofisini na akamwagiwa tindikali machoni. Polisi wakafungua kesi; mahakama ikatupa eti ni ugomvi wa mapenzi.

Twende Kenya. Jaramogi Oginga Odinga (baba wa Raila Odinga), licha ya kuwa kiongozi katika serikali ya Kenya, alishtuka serikali kuhusika kisiri kuua watu.

Sababu za kuamini hivyo ziko wazi. Odinga ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani kabla ya mwaka 1964 kuwa Makamu wa Rais alishangaa kuona uhusiano ukibadilika haraka na marafiki zake wakiuawa.

Mwaka 1965 Odinga alishtuka mshirika wake mkuu, mwanasiasa Mkenya mwenye asili ya Asia, Pio Gama Pinto akiuawa. Serikali ilipohojiwa ilikanusha kuhusika.

Baada ya kutafakari mauaji hayo na siasa zisizo na mwelekeo, mwaka 1966 alijiuzulu na kuunda chama cha Kenya People's Union (KPU). Mwaka 1967 alitunga kitabu kiitwacho Not Yet Uhuru yaani Uhuru Bado Kidogo kilichoeleza kwa kina siasa za Kenya.

Humo alieleza kwa kina kwamba mambo yaliyokuwa yanafanywa na wakoloni dhidi ya Waafrika, wanasiasa kutekwa, kupigwa na kuuawa kwa madai ya uhaini, ndiyo yalikuwa yanafanywa chini ya serikali yao dhidi ya raia.

Mwaka 1969 aliuawa Tom Mboya (Waziri wa Uchumi na Mipango), halafu Josiah Mwangi Kariuki (1975), na mwaka 1990 akauawa Robert Ouko (Waziri wa Mambo ya Kigeni), na wanaharakati wa haki za binadamu, Oscar Kamau Kingara (2009) na John Paul Oulo (2009).

Nani alimuua Ouko? John Troon, mchunguzi kutoka Scotland Yard alitaja wanasiasa kadhaa wakiwemo Nicholaus Biwott na Hezekiah Oyugi lakini serikali iliwakingia kifua. Alipoona mazingira ya kutoa ripoti kamili yanahatarisha usalama wake, Troon alirudi Uingereza.

Baadaye Kamati ya Bunge iliyoundwa kubaini muuaji wa Ouko, ilikwenda Uingereza kuonana na Troon ambaye alisema “Ouko aliuawa kwa amri ya serikali.”

Amri hiyo ya serikali “haikutolewa na mtu mwingine yeyote isipokuwa Rais Daniel arap Moi”.

Tena ilielezwa kuwa Ouko, alitekwa shambani kwake Koru, akasafirishwa hadi Nairobi, ambako aliuawa ikulu kisha wakaurudisha mwili wake shambani na kuuchoma moto. Ukatili ulioje?

Hapa Tanzania kuna hukumu zinazotia shaka. Mwaka 1995 walimfukuza Kombe wakamtwanga risasi kwa madai eti walimfananisha na jambazi aliyeiba gari la tajiri mmoja.

Kabla ya kumiminiwa risasi, Kombe alinyanyua mikono juu akiomba wasimdhuru, lakini wapi. Ikafunguliwa kesi eti ya kuua bila kukusudia, wakafungwa na sasa wako huru.

Unatakiwa kuwa na moyo mgumu kuhoji kilichowakuta Hanga, Othman Sharrif na wengineo. Nani aliondoa uhai wao, maradhi au mkono katili wa serikali?

Ili kila mmoja aridhike kwamba serikali haihusiki, Rais Kikwete aunde TUME HURU ya kuchunguza kadhia hiyo basi.
HII KITU NIMEIPATA KTK LINK HII  H A P A

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni