Mtayarishaji

Morning Star Radio

Jumapili, Juni 03, 2012

JE! CHAKULA KINAWEZA KUATHIRI AKILI YAKO?


(SOMA DANIELI 1 YOTE)

SOMA DANIELI 1 YOTE)
Amini usiamini, chakula kinaweza kuathiri akili yako, na afya yako ya kimwili na kiroho. Kwa maelezo zaidi juu ya somo hili la afya soma vitabu vya Afya na Lishe, kama vile Afya na Raha na Uponyaji wa Mungu ambamo zimefafanuliwa Kanuni 8 za Afya ----- Lishe bora, Mazoezi ya mwili, Hewa safi, Maji safi
na salama, Mwanga wa jua, Pumziko, Kiasi, na Kumwamini Mungu. Ukizifuata utaepukana na magonjwa mengi na kupunguza gharama ya matibabu. Yatabaki magonjwa yanayokuja kwa njia zingine zisizozuilika.

Chakula cha daraja la kwanza ambacho Mungu alimpa mwanadamu kilikuwa cha nafaka, kokwa na matunda (Mwanzo 1:29). Dhambi ilipoingia ilileta laana sio tu kwa viumbe vyote bali hata kwa ardhi. Kwa hiyo Mungu akamwongezea mwanadamu mboga za majani katika lishe yake ya awali (Mwanzo 3:18). Gharika ilikaa juu ya nchi kwa miezi mitano au siku 150 na kuharibu mimea yote (Mwanzo 7:24). Kwa hiyo Mungu akamwongezea mwanadamu katika lishe yake "nyama" kutoka kwa wanyama safi tu (Mwa. 8:3,4 imebainishwa na Law. 11:1-47; Kum. 14:1-21). Injini ya petroli hutumia petroli tu; injili ya dizeli ni dizeli tu. Ukitaka gari lako life weka dizeli katika injini ya petroli au petroli katika injini ya dizeli. Mtengenezaji ndiye anayejua gari lake litatumia mafuta gani, sio mtumiaji. Vile vile, Mungu anajua chakula kinachofaa kwa mwili wa mwanadamu, sio mwanadamu kujichagulia cho chote kuwa chakula. Wabishi wataharibu injini za magari yao (miili yao).

Mungu aliumba wanyama safi na wanyama najisi juma lile la kwanza la uumbaji. Kifo cha Yesu msalabani hakikuwa kwa kusudi la kuwabadilisha wanyama najisi kuwa wanyama safi, bali wanadamu wenye dhambi kuwa watakatifu. Wale wanaotaka kuwa watakatifu watajiepusha kula nyama inayotokana na wanyama najisi; lakini wale wasiotaka utakatifu wataswaga kila kitu (Law. 11:41,43,46,47; Kum. 14:1-4). Mungu hamlazimishi mtu, kama vile mtengenezaji wa injini ya gari asivyomlazimisha mtu kutumia
mafuta aliyopendekeza. Lakini matokeo mwilini ni ya hakika.

Kisa cha Petro katika Matendo 10:9-16 kimetafsiriwa chini yake katika fungu la 25 hadi 29. Hayo yalikuwa ni maono tu, si kitu halisi; hata hivyo Petro alikataa katakata kuchinja na kula wanyama najisi ingawa ni Mungu mwenyewe aliyemwamuru kufanya hivyo mara tatu. Mungu hana kigeugeu; alisema wanyama
najisi wasiliwe, basi, hawawezi kuliwa milele (Mal. 3:6; Zab. 89:34). Watu wanamsingizia bure Petro wanapochinja wanyama najisi na kula; yeye alikataa katakata. Lakini kuna adhabukali sana kwa wale wanaoendelea kula nguruwe, panya, na machukizo yote ya Mataifa (wapagani). Soma Isaya 65:2-6;
66:15-17).

Pombe haikuwa sehemu ya kinywaji ambacho Mungu alimpa mwanadamu; maji safi na salama ndicho kinywaji bora kuliko vyote kwa mwanadamu (Mithali 20:1; 23:29-35). Walevi hawataurithi ufalme wa Mungu (1 Kor. 6:9,10; Gal. 5:21). Kuna wengi wanaosema, "Mimi nakunywa sana, lakini silewi." Tatizo
la pombe sio kulewa tu, bali ni zile athari zinazotokana na kunywa pombe ambayo ina sumu mbaya ya alkoholi. Sumu hiyo huathiri vibaya moyo, mishipa ya fahamu, nyama za mwili na kadhalika. Mungu atamharibu mtu ye yote anayeuharibu mwili wake kwa makusudi kwa njia yo yote ile ----- pombe, tumbako, madawa ya kulevya, na kadhalika (1 Kor. 3:16,17). Pia kuna vinywaji vinavyopendwa na watu wengi aina ya 'Cola', Kahawa, na Majani ya Chai ambavyo huidhuru mishipa ya fahamu, ubongo na mwili.
Viepukwe.

Hebu sasa na tuwaangalie wale vijana wanne wa Kiebrania, mateka kutoka Yerusalemu, wakiwa katika jiji lile la Babeli mwaka ule wa 606 au 605 K.K. Walikuwa na umri kati ya miaka 18 na 20. Kutokana na hekima yao walichaguliwa kujiunga na vijana wengine wa Babeli katika Chuo cha Kishenzi [Kipagani] cha Babeli kwa mafunzo ya miaka mitatu. Wakapewa majina ya miungu ya Babeli ----- Danieli akaitwa Belteshaza, Hanania akaitwa Shadraka, Mishaeli akaitwa Meshaki, na Azaria akaitwa Abednego
(Dan. 1:6,7). Mfalme akaamuru wale chakula cha mfalme ili wanenepe na kuwa na akili nyingi. Kusudi lake lilikuwa zuri sana. Lakini, je! chakula kile cha mfalme ambacho kilikuwa na nyama najisi, kilikolezwa kwa viungo vingi vinavyodhuru mwili, na huenda kilikuwa na vileo kingeweza kuleta afya bora na akili safi? (Dan. 1:1-5). Vijana hao wanne wa Kiebrania walikuwa wamelelewa katika mazingira tofauti. Walifuata kanuni za afya  na chakula ambacho Mungu aliwapa wanadamu kula. Walijiepusha na nyama ya aina yo yote ile pamoja na divai (maji matamu ya zabibu) kwa vile wao walikuwa wanadhiri wa Bwana (Hesabu 6:1-5).
Kwa hiyo agizo hilo la mfalme kwao likawa mtihani mgumu sana.

"Danieli aliazimu moyoni mwake ya kuwa hatajitia unajisi kwa chakula cha mfalme, wala kwa divai aliyokunywa; basi akamwomba yule mkuu wa matowashi ampe ruhusa asijitie unajisi" (Dan. 1:8). Ni ujasiri ulioje! Ombi lake halikuwa rahisi kukubaliwa na msimamizi yule kwa vile angekatwa kichwa kama
wangeonekana wamekondeana (Dan. 1:10). Basi Danieli akamwambia, "Tafadhali utujaribu sisi watumishi wako muda wa siku kumi; na watupe mtama [nafaka, kokwa, mboga za majani, matunda] tule, na
maji tunywe. Kisha nyuso zetu zitazamwe mbele yako, na nyuso za wale vijana wanaokula chakula cha mfalme..." (Dan. 1:13). Akawakubalia ombi hilo. Je! mambo yalikuwaje kiafya baada ya siku zile kumi tu? "Nyuso zao zilikuwa nzuri zaidi [wanawake wanaohangaika na vipodozi vinavyodhuru afya wangezingatia hilo], na miili yao ilikuwa imenenepa zaidi, kuliko wale vijana wote waliokula chakula cha mfalme. Basi yule msimamizi akaiondoa posho yao ya chakula [cha mfalme], na ile divai waliyopewa wanywe, akawapa mtama [nafaka, kokwa, mboga za majani, matunda] tu" (Dan. 1:15,16).

Chakula cha matajiri au wafalme tunachokitamani sana hakileti afya mwilini. Chakula rahisi cha mimea na maji safi na salama ni lishe bora. Kwa akili safi na mwili wenye afya, ulionenepa kiafya sio kwa ugonjwa, tumia vyakula vya mimea na maji safi na salama, na kufuata Kanuni zile 8 za Afya. Wana sayansi wamegundua kuwa wale wanaokula vyakula vya mimea bila nyama wanaishi maisha marefu sana kuliko wanaokula nyama. Danieli naye aliishi zaidi ya miaka 80 kufikia kipindi cha utawala wa Koreshi (Dan. 1:21; 10:1). Hebu tuwafuatilie vijana wale wanne mwisho wa mafunzo yao ya miaka mitatu. Mfalme Nebukadreza aliwaonaje?

"Naye mfalme akazungumza nao; na miongoni mwao wote hawakuonekana waliokuwa kama Danieli, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria... Na katika kila jambo la hekima na ufahamu alilowauliza mfalme, akawaona kuwa wanafaa mara kumi zaidi ya waganga na wachawi waliokuwa katika ufalme wake" (Dan.1:19,20).

Kwa nini tuhangaike sana na suala la afya ya mwili wetu, je! maisha ya kiroho si bora zaidi? "Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako [kimwili], kama vile roho yako ifanikiwavyo" (3 Yohana 2). Wahenga walisema, "Akili timamu katika mwili wenye afya." Ni shauri la kuzingatiwa sana.
Kanuni ya Biblia ni hii: "Basi, mlapo, mnywapo, au mtendapo neno lo lote fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu" (1 Kor. 10:31). Tunawajibika kuitunza miili yetu katika hali ya afya nzuri kadiri iwezekanavyo (l Kor. 6:19,20; 1 Pet. 1:18,19; Rum.12:1,2). Suala la afya linahusu wokovu wetu. Mungu anaweza
kututumia kama Danieli (Dan. 1:17).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni