MAJIBU YAFANYAYO KAZI ni kipengele kinachoongelea masuala ya kiroho zaidi.
****************************************
“Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu
makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu
awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.” 2 Timotheo 3:16-17. Katika
Neno la Mungu kimo kila kitu cha muhimu kiwezacho kumkamilisha mtu wa Mungu. Ni
kama nyumba ya hazina iliyojaa bidhaa bora sana na za thamani.
“Lenye pumzi ya Mungu,” “ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu”
(fungu la 15), na kumfanya mtu wa Mungu, “awe kamili, amekamilishwa apate kutenda
kila tendo jema,” Kitabu hiki kipitacho vitabu vyote kina madai ya juu kabisa kwetu ili
tupate kukiangalia kwa kicho. Kukisoma kwa juu juu tu hakuwezi kukidhi [kutosheleza]
madai ambayo kinayo juu yetu, wala kutupatia sisi manufaa yanayoahidiwa humo.
Tungejitahidi kujifunza maana kamili ya lile Neno la kweli, na kuinywa kwa kina roho
ile iliyomo ndani ya Mausia hayo Matakatifu. Kusoma kila siku idadi fulani ya sura, au
kukariri kiasi fulani cha Maandiko kilichowekwa , bila kutafakari kwa makini maana ya
fungu hilo, kutaleta faida ndogo sana. Kujifunza kifungu cha maneno kimoja mpaka
maana yake imekuwa wazi mawazoni mwako, na uhusiano wake kwa mpango ule wa
wokovu uwe unaonekana wazi, kuna manufaa sana kuliko kusoma sura nyingi bila kuwa
na lengo lo lote linaloeleweka, wala kupata mafundisho yo yote yanayokujenga.
Hatuwezi kupata hekima toka katika Neno la Mungu bila kuwa na bidii ya dhati na
maombi katika kujifunza kwetu. Ni kweli kwamba sehemu fulani za Maandiko zi wazi
mno kuweza kukosewa; lakini ziko nyingine nyingi ambazo maana yake haiwezi
kuonekana upesi kwa kuziangalia kwa haraka, maana ile kweli haiwi juu. Ili kuelewa
maana ya vifungu vya maneno kama hivyo, ni lazima kulinganisha andiko na andiko; ni
lazima pawepo na utafiti wa makini na kutafakari kwa moyo wa maombi. Kujifunza
kama huko kutalipwa maridhawa. Kama mchimba machimbo anavyozigundua tabaka za
thamani za madini zilizofichwa chini ya uso wa nchi, ndivyo yule anayeendelea kwa bidii
kulichunguza Neno la Mungu kama hazina iliyositirika, atakavyoweza kuziona kweli zile
za thamani sana, ambazo zimefichwa kwa mtafutaji mzembe.
Lakini mafundisho hayo matakatifu ya Neno la Mungu usipoyafanya kuwa kanuni na
mwongozo wa maisha yako, kweli hiyo itakuwa si kitu kwako. Kweli inafaa tu wakati
ule inapotekelezwa kwa matendo katika maisha yako. Kama Neno la Mungu
linaishutumu tabia yako moja unayoipenda, hisia yako unayoitunza moyoni mwako, roho
uliyoidhihirisha, basi, wewe usigeuke na kumpa kisogo mshauri wako huyo mtakatifu
[Neno la Mungu], bali uupe kisogo uovu ule unaoufanya na kumruhusu Yesu kukusafisha
na kukutakasa moyo wako. Ungama makosa yako, na kuachana nayo kabisa na kwa nia
thabiti, ukiziamini ahadi za Mungu, na kuonyesha imani yako kwa matendo yako. Kama
kweli za Biblia zinafumwa pamoja na matendo ya maisha yako, basi, zitaweza kuyainuamawazo yako toka katika hali yake ya kuipenda dunia pamoja na upotovu wake. Wale
wanaoyajua sana Maandiko watakuwa ni wanaume na wanawake ambao mvuto wao una
nguvu ya kuwainua watu. Katika kuzichunguza kweli hizo za Mbinguni zilizofunuliwa,
Roho wa Mungu huunganishwa na moyo wako kwa karibu sana.
Kuyaelewa mapenzi ya
Mungu yaliyofunuliwa huukuza ubongo, huupa mawazo bora, na kuupa nguvu mpya,
kwa kuuleta uwezo wake mbalimbali katika mgusano na ile kweli kubwa mno ajabu.
Hakuna somo liwezalo kuupa ubongo nguvu yake na kuiimarisha akili kama kulivyo
kujifunza Neno la Mungu. Hakuna kitabu kinginecho chote chenye uwezo mkubwa mno
katika kuyaadilisha mawazo, kuupa nguvu uwezo wa akili, kama ilivyo Biblia, ambayo
inazo kweli bora kabisa. Kama Neno la Mungu lingesomwa linavyopaswa kusomwa,
basi, tungeweza kuuona upana wa mawazo, uthabiti wa nia, ubora wa tabia, kama ule
unaoonekana kwa nadra sana katika nyakazi hizi.
Walakini, kujifunza Biblia kunapewa nafasi ya pili katika mawazo yetu, na kwa ajili
hiyo, hasara kubwa inapatikana. Ufahamu wetu unafuata usawa wa mambo yale
unayoyazoea. Kama wote wangeifanya Biblia kuwa somo lao, tungeweza kuwaona watu
waliokua vizuri, wenye uwezo wa kufikiri kwa kina zaidi, ambao wangeonekana kuwa na
ujuzi mkubwa kuliko wale waliosoma kwa bidii sayansi mbalimbali pamoja na historia
za ulimwengu huu, ambao wanaiacha Biblia. Biblia humpa mtafutaji wa ile kweli
nidhamu ya hali ya juu kiakili, naye anapotoka katika kutafakari mambo hayo ya Mungu,
nguvu zake za akili zikiwa zimesitawishwa; nafsi yake inanyenyekezwa, wakati Mungu
na kweli yake iliyofunuliwa kwake inapotukuzwa. Ni kwa sababu watu hawazifahamu
historia za thamani zilizo katika Biblia, ndiyo maana kuna hali ya kumtukuza mno
mwanadamu na heshima ndogo mno hutolewa kwa Mungu.
Biblia inacho kile kiwezacho kumfanya Mkristo kuwa na nguvu ya kiroho na kiakili.
Mtunga Zaburi asema hivi, “Kuyafafanusha maneno yako kwatia nuru, na
kumfahamisha mjinga.” Zaburi 119:130. Biblia ni kitabu cha ajabu. Ni historia
inayotufunulia sisi mambo ya karne zile zilizopita. Pasipo kuwa na Biblia, sisi
tungekuwa tumeachwa kufuata dhana mbalimbali na hadithi za uongo kwa habari ya
matukio ya vizazi vile vilivyopita.
Ni unabii unaolifunua pazia la siku zijazo. Ni Neno la
Mungu, liufunualo mpango ule wa wokovu, ambalo linatuonyesha njia ile ambayo kwayo
sisi tunaweza kuikwepa mauti ile ya milele, na kujipatia wema wa milele na uzima wa
milele. Katika vitabu vyote vinavyoigharikisha [vinavyoijaza] dunia hii, haidhuru viwe
vya thamani ilioje, Biblia ni Kitabu kipitacho vitabu vyote, inastahili kabisa kuwa somo
letu na kupewa heshima. Haitupatii sisi historia ya ulimwengu huu tu, bali maelezo ya
ulimwengu ule ujao. Ina mafundisho yahusuyo maajabu ya malimwengu mbalimbali;
inatufunulia katika ufahamu wetu tabia ya Mwasisi yule wa mbingu na nchi. Ndani yake
umo ufunuo wa Mungu kwa mwanadamu.
Kuvichunguza vitabu vya falsafa na sayansi hakuwezi kuiletea akili na maadili kile
ambacho kujifunza Biblia kunaweza kutuletea, mradi tu kiwekwe katika matendo yetu.
Yule anayejifunza Biblia anaongea na wazee wa zamani pamoja na manabii. Anagusana
na ile kweli iliyovikwa mavazi ya lugha ya heshima, ambayo ina mvuto wenye nguvu
unaoupendeza moyo, na kuyainua mawazo toka katika mambo ya dunia hii kwenda
kwenye utukufu ule wa maisha ya baadaye ya milele.
Ni hekima gani ya mwanadamu
inayoweza kulinganishwa na ufunuo wa utukufu wa Mungu. Mwanadamu mwenye
maisha mafupi, asiyemjua Mungu, anajitahidi kuipunguza thamani ya Maandiko, akidaikwamba, maarifa yake ya sayansi anayodhania kuwa anayo, hayawezi kupatana na
Neno la Mungu; lakini Neno la Mungu ni taa ya miguu yetu na mwanga wa njia yetu.
Wale wanaojigamba kwamba wanayo hekima nyingi kuliko ile ifundishwayo katika
Neno la Mungu wanahitaji kunywa kwa kina zaidi katika chemchemi hiyo ya maarifa, ili
wapate kuuona ujinga wao ulivyo hasa.
Wanadamu hujisifu wenyewe kwa hekima
waliyo nayo, wakati hekima hiyo ni upumbavu mtupu. Hebu na asiwepo mtu awaye yote
anayejidanganya mwenyewe. “Mtu akijiona kuwa mwenye hekima miongoni mwenu
katika dunia hii, na awe mpumbavu, ili apate kuwa mwenye hekima. Maana hekima ya
dunia hii ni upuzi mbele za Mungu. Kwa maana imeandikwa, Yeye ndiye awanasaye
wenye hekima katika hila yao.” 1 Wakorintho 3:18-19. Ujinga mkubwa mno
unaowaletea laana wanadamu hivi sasa ni ujinga wa kukosa kuyajua masharti ya
Sheria ya Mungu [Amri Kumi – Kut. 20:3-17] ambayo yanawafunga wanadamu wote;
na ujinga huo ni matokeo ya kudharau kulichunguza Neno la Mungu. Ni mpango wake
Shetani kuyashughulisha mno mawazo kiasi cha kuwafanya wanadamu kukiacha Kitabu
hicho Kikuu cha Mwongozo, na hivyo kuwafanya waongozwe katika njia ile ya uasi
[uvunjaji wa Amri Kumi – Yak. 2:10-12] na maangamizi.
Biblia haipewi heshima na kuwekwa mahali pake inapostahili miongoni mwa vitabu
vya ulimwengu huu, japokuwa kuisoma kuna umuhimu usio na kifani kwa roho za
wanadamu. Katika kuzichunguza kurasa zake mawazo yetu huziona mandhari [picha]
zile tukufu za milele. Twamwona Yesu, Mwana wa Mungu, akija katika dunia yetu, na
kuingia katika pambano la ajabu ambalo limezivunjilia mbali nguvu zile za giza. Lo!ni
ajabu jinsi gani, ni jambo ambalo karibu halisadikiki kabisa kwamba Mungu yule wa
milele angeweza kukubali Mwana wake apate kudhalilishwa kiasi kile, ili sisi tupate
kuinuliwa juu na kuketi pamoja naye katika kiti chake cha enzi!Hebu kila mwanafunzi
wa Maandiko na atafakari ukweli huo mkuu, ndipo hatatoka katika kujifunza Biblia
pasipo kutakaswa, kuinuliwa juu na kuadilishwa.
Ile kweli itafunuliwa akilini mwake na
kutumiwa na Roho wa Mungu katika moyo wake. Kwa njia ya kuunganishwa na Mungu,
Mkristo atakuwa na mawazo safi na mapana zaidi, yasiyopendelea kufuata maoni yake
mwenyewe aliyokuwa nayo hapo kwanza. Uwezo wake wa kupambanua mema na
mabaya utapenya ndani zaidi, uwezo wake wa akili utakuwa na uwiano mzuri zaidi.
Akili yake, ikitumika katika kuzitafakari zile kweli tukufu, itapanuka, na katika kujipatia
maarifa yale ya mbinguni ataweza kuujua vizuri zaidi udhaifu wake alio nao, naye atakua
katika imani na katika unyenyekevu wake wa moyo. Usikivu mdogo tu ukitolewa kwa
Neno la Mungu, mashauri ya Mungu huwa hayazingatiwi, maonyo yanayotolewa huwa
kazi bure, neema na hekima ya mbinguni haitafutwi ili dhambi zile zilizopita zipate
kuepukwa na kila waa la ufisadi lipate kusafishwa katika tabia yetu.
Daudi aliomba,
akasema, “Unifahamishe njia ya mausia yako [yaani, amri zako – KJV].” “Unifumbue
macho yangu niyatazame maajabu yatokayo katika Sheria yao [Amri Kumi].” Zaburi
119:27,18.
Ipo kazi kubwa ya kufanywa na mwanafunzi wa Biblia mwenye bidii; kwa sababu
vito vya thamani vya ile kweli vinatakiwa kukusanywa na kuletwa juu, kisha vinapaswa
kutengwa mbali na urafiki wo wote na makosa [mafundisho potofu]. Ingawa Biblia ni
ufunuo utokao mbinguni, hata hivyo, wengi hawayaelewi mafundisho yake ya mbinguni.
Tunapaswa kugundua maono mapya ya ile kweli katika Agano la Kale na Agano Jipya,
hatuna budi kukiona kina na upana upitao kiasi wa zile kweli tunazofikiri kwamba
tunazijua, lakini ambazo sisi tuna ujuzi wake wa juu juu tu. Yule anayeyachunguzaMaandiko kwa bidii ataona kwamba mwafaka upo kati ya sehemu mbalimbali za Biblia;
atagundua uhusiano wa kifungu kimoja cha maneno na kile kingine, na thawabu ya taabu
yake [ya kujitahidi kukichunguza] itakuwa ya thamani kubwa mno.
Katika eneo lote la ufunuo huo zimetawanyika chemchemi za furaha, amani na
shangwe za ile kweli ya mbinguni. Chemchemi hizo za furaha zinaweza kufikiwa na kila
mmoja atafutaye. Maneno yale ya Uvuvio, yakifikiriwa sana moyoni, yatakuwa kama
vijito vinavyotiririka kutoka katika mto ule wa maji ya uzima. Mwokozi wetu aliomba
kwamba akili za wafuasi wake zipate kuzinduliwa ili kuyaelewa Maandiko hayo. Kila
tunapojifunza Biblia kwa moyo wa maombi, Roho Mtakatifu huwa karibu nasi
kutufunulia maana ya maneno yale tusomayo. Mtu yule ambaye akili yake imetiwa nuru
kwa kulifafanua Neno la Mungu, hatajisikia tu kuwa anapaswa kutafuta kwa bidii ili
apate kulielewa Neno lile, bali kwamba anapaswa kuwa na ujuzi bora wa sayansi zile
nyingine. Atajisikia kwamba ameitwa kwa mwito ule mkuu katika Kristo Yesu. Kadiri
mwanadamu anavyounganishwa kwa karibu sana na lile Chimbulo la maarifa yote na
hekima, ndivyo kadiri atakavyojisikia kwamba hana budi kusonga mbele katika kujipatia
mambo yale ya kiakili na kiroho. Roho Mtakatifu, kwa njia ya ile kweli ya Mungu,
huuhuisha uwezo ule wa kiroho uliokufa na kuuvuta moyo kuelekea mbinguni.
Basi, chukua Biblia yako na kujiweka mbele za Baba yako wa Mbinguni, ukisema,
“Unitie nuru; unifundishe kweli ni nini.” Bwana ataifikiria sala yako, na Roho Mtakatifu
ataitia kweli hiyo moyoni mwako. Katika kuyachunguza Maandiko wewe mwenyewe,
utakuwa umejiimarisha katika imani. Ni jambo la maana sana kwamba uweke moyoni
mwako akiba ya kweli hizo za Mungu. Unaweza kujikuta uko mahali ambako hutapata
nafasi ya kukutana na watoto wa Mungu. Unahitaji kuzificha hazina za Neno la Mungu
moyoni mwako, ili upinzani utakapokuja dhidi yako, upate kulipima kila jambo kwa
Maandiko hayo.
Kweli ni ya milele, na kupambana kwake na uongo [mafundisho potofu]
kutaudhihirisha tu uwezo wake. Kamwe tusikatae kuyachunguza Maandiko pamoja na
wale ambao tunayo sababu ya kuamini kwamba wanataka kujua kweli hiyo ni nini.
Tuseme ndugu mmoja anashikilia maoni yaliyo tofauti na yako, naye anakuja kwako, na
kupendekeza kwamba wewe uketi chini pamoja naye na kulichunguza jambo lile katika
nuru ya Maandiko; je!ungesimama ukiwa umejazwa na chuki bila sababu na
kuyashutumu mawazo yake, na wakati uo huo ukiwa unakataa kumpa usikivu wako
usiopendelea upande wo wote? Njia pekee sahihi kwetu sisi kama Wakristo ingekuwa ni
ile ya kuchunguza msimamo uliotolewa katika nuru ya Neno la Mungu, ambalo litaifunua
kweli na kuufichua uongo.
Kuyadhihaki mawazo yake kusingeweza kuudhofisha
msimamo wake, ingawa [yale usemayo] yangekuwa ni ya kweli. Hebu kilete kila kitu
kwenye Biblia; kwa maana hiyo peke yake ndiyo kanuni ya imani na mafundisho ya
dini. Hatuna budi kujifunza ile kweli sisi wenyewe; tusimtegemee mtu awaye yote
kufikiri kwa niaba yetu, haidhuru awe ni nani au awe na cheo gani. Hatupaswi
kumwangalia mwanadamu ye yote kama kiongozi mkamilifu [asiye na dosari]
aliyewekwa kwa ajili yetu. Tunapaswa kushauriana pamoja na kunyenyekeana; lakini
wakati uo huo hatuna budi kumwangalia Mungu kwa ajili ya kututia sisi nuru ile ya
mbinguni, ili kila mmoja wetu apate kukuza tabia ile itakayoweza kushinda katika jaribio
la siku ile kuu.
Sisi tunaishi katika siku za mwisho, wakati makosa [mafundisho ya uongo] yaliyojaa
udanganyifu wa hali ya juu yanapokelewa na watu na kusadikiwa, wakati ile kweli [Nenola Mungu – Yn. 17:17] inapotupiliwa mbali. Wengi wanachukuliwa na mkondo wa maji
na kuingia katika giza [la ujinga] na ukafiri, wanaikosoa Biblia, wanaleta mavumbuzi ya
kishirikina [uchawi], wanaleta nadharia zisizoungwa mkono na Maandiko, pamoja na
dhana zinazotokana na falsafa ya kipumbavu; lakini ni jukumu la kila mmoja wetu
kujitahidi kupata ujuzi kamili wa Maandiko. Umuhimu na faida ya kujifunza Biblia
haviwezi kusifiwa mno. Katika kuyachunguza Maandiko mawazo yetu huongozwa
katika kuifikiria sana ile kafara ya Kristo isiyo na kikomo katika kutupatanisha sisi.
Tunapouona upendo wake, tunapotafakari juu ya kujidhili kwake na mateso yake, roho
ile ile ya kujikana nafsi na kujitoa mhanga kwa faida ya wengine inaamshwa ndani ya
mioyo yetu. Tunapomtazama Yesu kwa jicho la imani, tuta“badilishwa tufanane na
mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, kama vile utukufu utokao kwa Bwana, aliye
Roho.” 2 Wakorintho 3:18.
Bibi E. G. White, The Power of the Word, au Kichwa cha makala ya awali ni
“Apples of Gold Library No. 10.”
***********************************************
Kwa sababu ya upekee na unyeti wa siku, Sio vibaya tukibadilishana mawazo na kuambizana yaliyomuhimu katika maisha hasa ya kiroho.
Na huu utakuwa ni mfululizo kwa kila siku kama hii ya leo...
(Ninamaanisha JumaMosi)
Pamoja na kwamba weeengi wanaamini hii ni kweli, lakini kweli halisi jionee mwenyewe ambapo Walter Pearson anajambo la kutwambia.
AMANI KWAKO.
Amani kwako pia NGULI na asante kwa SHULE hii!
JibuFutaIla nasikia UWEZO wa NENo ni siri ya mafanikio ya hata WANAMAZINGAOMBWE ,...
... na pia hata UCHAWI kwa WACHAWI ni jambo la KIROHO!
Ni angalizo tu hili MKUU!
Ahsante sana Paulina.Mungu akubariki.
JibuFuta