Mtayarishaji

Morning Star Radio

Jumatatu, Agosti 01, 2011

TOKENI MIJINI... SEHEMU YA 7 HADI 9

SEHEMU YA SABA

Kuongozwa na Maongozi ya Mungu

Mungu Anapoifungua Njia

Wakati umefika, ambapo, kadiri Mungu anavyoifungua njia, familia hazina budi kutoka mijini.

Watoto wapelekwe kule shamba [vijijini]. Wazazi na wajipatie mahali panapofaa kulingana na

fedha walizo nazo zitakavyoruhusu. Ingawa nyumba ile iliyojengwa inaweza kuwa ndogo, hata

hivyo, pangekuwapo na shamba linaloweza kulimwa kuambatana nayo. ----- Manuscript 50, 1903.

Mungu Atawasaidia Watu Wake

Wazazi wanaweza kujijengea nyumba ndogo huko shamba [vijijini], na kuwa na mashamba ya

kulima, ambamo wanaweza kuwa na viunga vya miti ya matunda, na kupanda mboga za majani

pamoja na matunda madogodogo ili kuchukua mahali pa nyama, ambayo inaichafua sana damu

inayopita katika mishipa na kuleta uzima. Mahali hapo watoto hawatazungukwa na mivuto ile

miovu ipatikanayo katika maisha yale ya mjini. Mungu atawasaidia watu wake kupata makazi

kama hayo nje ya miji [wakimwomba]. ----- Medical Ministry, uk. 310. (1902)

Kusaidia Kuifungua Njia

Wakati unapozidi kusonga mbele, watu wetu wengi zaidi na zaidi watalazimika kuihama miji.

Kwa miaka mingi tumeagizwa ya kwamba ndugu na dada zetu, na hasa familia zile zenye watoto,

wangefanya mpango wa kuondoka mijini kwa kadiri njia inavyofunguka mbele yao na

kuwawezesha kufanya hivyo. Wengi watalazimika kufanya kazi ngumu kwa bidii ili kusaidia

kuifungua njia. Lakini mpaka hapo itakapowezekana kwao kuhama, kadiri wanavyoendelea kubaki

humo, wangefanya bidii kubwa sana kufanya kazi ya umishonari, haidhuru eneo la mvuto wao liwe

dogo jinsi gani. ----- Review and Herald, Sept. 27, 1906.

Ushauri na Onyo Kwa Wale Wanaotarajia Kuondoka Mijini

[Barua hii iliandikwa Desemba 22, 1893, kuijibu barua iliyotoka kwa kiongozi maarufu wa Battle

Creek, akimjulisha Bibi White kuwa kama itikio lao kwa onyo lile linalowataka watu wetu kuhama

kutoka Battle Creek, "kati ya watu mia moja na mia mbili" hivi walikuwa wanajiandaa kuondoka

"kwa haraka iwezekanavyo." -----

WAKUSANYAJI WA MAANDIKO.]

Ndugu yangu, barua yako inaniambia kwamba wapo wengi waliopata mwamko mkubwa wa

kuondoka Battle Creek. Ipo haja, haja kubwa, ya kazi hiyo kufanyika, na kufanyika sasa. Wale

wanaojisikia kuhama hivi mwishoni hebu isiwe kwa kukurupuka, kwa msisimko, au bila kufikiri,

au kwa njia ambayo hatimaye watajuta sana kuhama kwao....

Angalieni sana pasiwepo na kuhama kunakofanywa bila kufikiri katika kulitii onyo hilo la kuhama

kutoka Battle Creek. Msifanye jambo lo lote bila kuitafuta hekima toka kwa Mungu, ambaye

ameahidi kuwapa kwa ukarimu wale wote wamwombao, na ambaye hakemei [Yakobo 1:5]. Yale

yote ambayo mtu ye yote anaweza kufanya ni kuwapasha habari tu na kutoa ushauri wake, kisha

kuwaacha wale wanaoamini kwa dhati kuhusu wajibu wao wa kuhama, wakiwa chini ya uongozi

wake Mungu, kufanya hivyo; mioyo yao yote ikiwa imefunguliwa wazi ili wapate kujifunza na

kumtii Mungu.

Mimi nasumbuka sana moyoni mwangu kufikiri kwamba huenda wapo hata baadhi ya waalimu

[wachungaji, n.k.] wetu ambao wanahitaji kuwa na busara zaidi ili waweze kufikiria pande zote [za

jambo hilo]. Wajumbe wale wanaouchukua ujumbe huo wa rehema kwa ulimwengu wetu, ambao

wanategemewa na watu wetu, wataombwa kutoa mawaidha [maoni] yao. Tahadhari kubwa haina

budi kutumika kwa upande wa watu hao ambao hawana uzoefu halisi wa maisha ya kujitegemea

[vijijini] kwa kufanya kazi [kwa mikono yao], na ambao watakuwa hatarini kutoa mawaidha yao,

wasijue mawaidha yao hayo yatasababisha watu wengine kufanya kitu gani.

KIPAWA CHA KUTOA USHAURI

Watu wengine wanaona mbali katika mambo mengi, hao wanao uwezo wa kutoa ushauri. Ni

kipawa cha Mungu. Katika nyakati zile ambazo kazi ya Mungu inahitaji maneno ya busara na ya

dhati, na yale yaliyo thabiti, hao wanaweza kusema maneno fulani ambayo yatawafanya watu wale

waliochanganyikiwa pamoja na wale walio gizani [wasioelewa kitu], kuiona kwa ghafula, kama

vile nuru ya mwanga wa jua inavyomulika ghafula, njia ile wanayopaswa kuifuata katika jambo lile

lililowajaza mashaka mengi na kuifadhaisha sana mioyo yao wakati walipokuwa wakifanya

uchunguzi wao uliowachukua majuma mengi na miezi mingi. Ufumbuzi upo, yaani, ufyekaji wa

njia ile iliyo mbele yao, na Mungu ameruhusu mwanga wake wa jua kuingia mawazoni mwao, nao

wanaona ya kuwa maombi yao yamejibiwa, yaani, njia yao iko wazi. Lakini basi, mawaidha fulani

yanaweza kutolewa bila kufikiri, yakisema ----- tokeni tu Battle Creek, wakati hakuna maelezo yo

yote yaliyofafanuliwa vizuri kuhusu maendeleo gani watakayofanya katika maisha yao ya kiroho

kwa ajili yao wenyewe au kwa ajili ya wengine kwa kuichukua hatua hiyo [ya kuhama].

FIKIRIENI KWA MAKINI SANA KILA HATUA YA KUHAMA KWENU

Hebu kila mmoja awe na muda wa kutosha wa kufikiria [jambo hilo] kwa makini [uangalifu] sana;

asije akafanana na mtu yule aliyetajwa katika mfano [wa Yesu] aliyeanza kujenga, kisha

akashindwa kumaliza. Kuhama ko kote kusifanyike isipokuwa kama kuhama huko na matokeo

yake yote yamefikiriwa kwa makini sana ----- yaani, kila jambo limepimwa kuona uzito wake...

Kwa kila mtu kazi ilitolewa kulingana na uwezo wake. Basi, asihame akiwa na mashaka, bali

ajizatiti, na wakati uo huo akiwa ananyenyekea kwa kumtegemea Mungu.

Huenda wakawapo watu ambao watataka kuharakisha kufanya jambo fulani, na kujiingiza katika

shughuli fulani ambayo hawaijui kabisa. Mambo hayo Mungu hataki. Fikiri kwa moyo mnyofu,

kwa maombi, ukijifunza Neno [la Mungu] kwa makini sana na kwa maombi, akili yako na moyo

wako vikiwa tayari kuisikiliza sauti ya Mungu.... Kuyajua mapenzi ya Mungu [katika suala hili] ni

jambo kubwa.

MIPANGO ILIYOPANGWA VIZURI INATAKIWA

Nayatoa maneno haya kwa kanisa lile lililoko kule Battle Creek ili lipate kutembea katika

mashauri ya Mungu. Haja ipo ya kuhama kwenu ----- yaani, wengi wenu kuhama kutoka Battle

Creek ----- tena, ipo haja pia ya ninyi kuwa na mipango iliyopangwa vizuri juu ya kile

mtakachofanya mtakapohama toka Battle Creek. Msiende kwa kukimbia, bila kujua

mnachofanya.... Laiti kama wangekuwapo majenerali wenye hekima, wanaowafikiria wengine,

watu wale wanaoyachunguza mambo kwa kuangalia kila upande, watakaokuwa washauri salama,

ambao kidogo wanajua kile kilichomo ndani ya mwanadamu, wale ambao wanajua kuongoza na

kushauri katika kicho chake Bwana.

HATARI INAAMBATANA NA UZOEFU MPYA

Nimekwisha kuona kwamba hatari inaambatana na kila awamu mpya ya uzoefu kanisani, kwa

sababu wengine wanayasikia mambo hayo kwa moyo wenye kusisimka sana. Wakati waalimu

[wachungaji, n.k.] wengine wanaweza kuwa imara upande ule wa kufundisha mafundisho ya

Biblia, si wote watakaokuwa wamepata uzoefu wa maisha ya kujitegemea, si wote

watakaowashauri wale waliochanganyikiwa kwa hakika na usalama. Hawaitambui hali hiyo ya

kutatanisha ambayo haina budi kuja kwa kila familia itakayofanya mabadiliko hayo. Kwa hiyo,

wote wawe waangalifu sana kuchunga maneno yao wanayosema; kama hawayajui mawazo ya

Mungu katika baadhi ya mambo, basi, wasiseme kabisa kwa kukisia-kisia tu au kwa kudhani kuwa

mambo hayo yako hivyo. Kama hawajui kitu cho chote kilicho dhahiri, hebu na waseme hivyo, na

kuwaacha watu kila mmoja peke yake wapate kumtegemea Mungu. Hebu maombi mengi

yafanyike, hata kwa kufunga, ili mtu ye yote asije akahama akiwa gizani [hajui la kufanya], bali

ahame akiwa nuruni [anajua la kufanya] kama vile Mungu alivyo nuruni....

HAMENI KWA HADHARI

Hebu pasiwepo na kitu cho chote kinachofanywa bila utaratibu, isije ikatokea hasara kubwa au

kupoteza mali kwa sababu ya hotuba motomoto zilizotolewa zenye kujaa misisimko ndani yake

ambazo zinaamsha shauku ambayo haimo katika mpangilio wa Mungu, hata ushindi ule uliokuwa

wa lazima kupatikana uweze kugeuka na kuwa kushindwa kunakotokana na kukosa utulivu wa

kusimamia mambo vizuri na kuyafikiria vizuri, na kujenga juu ya kanuni na makusudi yaliyo

imara. Hebu na pawepo na uongozi wa busara katika jambo hilo, na wote wapate kuhama chini ya

uongozi ule wenye hekima wa Mshauri yule asiyeonekana, ambaye ni Mungu. Mambo ya

kibinadamu yatajitahidi kutawala, na huenda pakawa na kazi iliyofanyika ambayo haina sahihi

[idhini] ya Mungu. Basi, namsihi kila mtu asiwaangalie washiriki hao wa kibinadamu kwa nia na

imani thabiti sana, bali amwangalie kwa bidii nyingi sana Mungu, mshauri mmoja aliye a hekima.

Wekeni njia zenu zote na mapenzi [nia] yenu ili yapatane na njia za Mungu na mapenzi yake....

MATOKEO YA HATUA ZA HARARA

Endapo wengine watahama kwa haraka na kukimbia toka Battle Creek, halafu wakajikuta

wameingia katika hali ya kukata tamaa, basi, watatoa shutuma zao, sio juu yao wenyewe, kwa

kuhama kwao bila kutumia busara, bali juu wa wengine, ambao watawalaumu kuwa walitia

shinikizo lao juu yao [mpaka wakawa wamehama]. Kutibuliwa kwa mipango yao yote na

kushindwa kwao kutawafanya wawarudishie shutuma zote wale ambao wasingestahili kupewa sifa

mbaya kama hizo....

Sasa, hivi sasa, ndio wakati ambao hatari zile kubwa za siku za mwisho zinazidi kuongezeka sana

kutuzunguka pande zote, tunahitaji watu wenye hekima kuwa washauri wetu, sio watu wale

watakaoona kwamba ni wajibu wao kuwasisimua watu na kuleta machafuko, bali ni wale wawezao

kutoa mashauri yao ya busara na kuratibu na kupanga mipango ili kwamba kila msisimko

unaotokea upate kuleta mpangilio mzuri kutoka katika machafuko yaliyopo, na kuleta raha na

amani kwa njia ya kulitii Neno la Bwana. Hebu kila mtu na apatikane mahali pake panapomfaa

hasa, ili apate kumfanyia Mungu kazi fulani, kulingana na uwezo wake aliopewa....

Kwa jinsi gani jambo hilo litaweza kufanyika? "Jitieni nira yangu," asema Yesu Kristo, yule

aliyewanunua ninyi kwa damu yake ya thamani, ninyi ambao ni watumishi na mali yake, "mjifunze

kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;

kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi." Endapo kila mmoja atakuja kwa

Yesu akiwa na moyo ulio tayari kufundishwa, moyo wenye toba, hapo ndipo atakuwa katika hali ya

kiakili ya kuweza kufundishwa na kujifunza kwa Yesu na kuyatii maagizo yake....

WEKENI KILA MPANGO MLIO NAO MBELE ZAKE MUNGU

Hatuwezi kuwa na imani dhaifu sasa; hatuwezi kuwa salama kwa kuwa na mtazamo ulio mlegevu,

wa kivivu, na wa kizembe. Kila chembe ya nguvu yetu inapaswa kutumika, na fikira kali, tulivu,

zenye kina zinapaswa kutumika. Hekima ya mjumbe ye yote wa kibinadamu haitoshi katika

kupanga mipango na kubuni mbinu kwa wakati kama huu. Wekeni kila mpango mlio nao mbele

zake Mungu kwa kufunga pamoja na kujinyenyekeza nafsi zenu mbele zake Bwana Yesu, na

kuzikabidhi njia zenu kwa Bwana. Ahadi ya hakika ni hii, "Naye atayanyosha mapito yako

[Atakuongoza katika njia zako - Mithali 3:5,6]. Yeye hana kikomo katika uwezo wake wa kusaidia.

Mtakatifu wa Israeli, anayeliita jeshi lote la mbinguni kwa majina yake, na kuzishikilia nyota za

mbinguni mahali pake, anawatunza ninyi kila mmoja peke yake....

Ningependa kwamba wote wapate kutambua uwezekano na mwelekeo uliopo kwa wale wote

wanaomfanya Kristo kuwa utoshelevu wao na tegemeo lao. Uhai ule uliofichwa pamoja na Kristo

katika Mungu daima unalo kimbilio; mtu huyo anaweza kusema, "Nayaweza mambo yote katika

yeye anitiaye nguvu."

Jambo hili nawaachieni mikononi mwenu; kwa maana nimekuwa na wasiwasi na kusumbuka sana

kwa ajili ya hatari zile zinazowashambulia wote walioko huko Battle Creek, ili wasije wakahama

bila kuwa na tahadhari kubwa na [kwa kufanya hivyo] kumpa yule adui yetu faida kubwa. Jambo

hilo halipaswi kuwa hivyo, maana kama tukienda kwa unyenyekevu na Mungu wetu, basi,

tutakwenda salama. ----- Letter 45, 1893.


SURA YA NANE

Vituo Vyetu vya Taasisi Kuwa Mbali na Msongamano wa Watu

Mahali Panapofaa Kujenga Taasisi Zetu

Agizo [lile lile] bado linazidi kutolewa, Tokeni mijini. Jengeni hospitali zenu, shule zenu, na ofisi

zenu mbali na vituo vyenye watu wengi. Wengi kwa wakati huu wanaomba sana ili wapate kubakia

mijini, lakini wakati utakuja, muda si mrefu kuanzia sasa, ambapo wale wote wanaotaka kuziepuka

tamasha na sauti hizo za uovu watakapohama na kwenda shamba [vijijini]; kwa maana uovu na

uchafu utaongezeka kwa kiwango ambacho mazingira yote ya mjini yataonekana kana kwamba

yamechafuliwa. ----- Letter 26, 1907.

Kuepuka Majaribu na Ufisadi

Wengine wameshangaa kwa nini ofisi yetu ya uchapishaji inatakiwa kuhamishwa toka Oakland

kwenda Mountain View. Mungu amekuwa akiendelea kuwaita watu wake kuondoka mijini. Vijana

wetu ambao wamefungamana na taasisi zetu hawapaswi kuwekwa mahali pale watakapoweza

kukabiliwa na majaribu na ufisadi unaoonekana katika miji mikubwa. Mountain View

pameonekana kuwa ni mahali panapofaa kwa ofisi yetu ya uchapishaji. ----- Manuscript 148, 1905.

Nyakati za Dhoruba Zi Mbele Yetu

Janga hilo [la kuteketezwa kwa moto jengo la Review and Herald] linaweza kuleta mabadiliko

dhahiri katika mambo yetu. Natumaini kwamba ndugu zetu hao watalizingatia fundisho hilo

ambalo Mungu anataka kuwafundisha, na ya kwamba hawatarudia kuijenga tena nyumba ya

uchapishaji pale Battle Creek. Mungu anamaanisha kwamba sisi hatutakaa mijini; maana zinakuja

nyakati za dhoruba kali sana mbele yetu. ----- Letter 2, 1903.

Mahali Wanapoweza Kufundishwa Kwa Ufanisi Vijana Wetu

Mungu ametuma kwetu onyo baada ya onyo ya kwamba shule zetu na nyumba zetu za uchapishaji

pamoja na hospitali zetu hazina budi kujengwa nje ya mji, mahali wanapoweza kufundishwa kwa

ufanisi vijana wetu kuhusu kweli ni nini. Asiwepo mtu ye yote anayezitumia Shuhuda [zangu]

kutetea ujenzi wa shughuli zetu kubwa za kibiashara mijini. Msiitangue nuru iliyokwisha kutolewa

kwetu juu ya somo hilo.

Watu watainuka [watatokea] wakisema mapotovu, wakifanya kazi yao kupinga mambo yale yale

ambayo Bwana anawaongoza watumishi wake kufanya. Lakini wakati umewadia kwa wanaume na

wanawake kufikiri kwa kulinganisha chanzo cha jambo na matokeo yake. Tumechelewa mno,

tumechelewa mno kuanzisha mashirika makubwa ya biashara mijini ----- tumechelewa mno

kuwaita vijana wetu wa kiume na wa kike watoke vijijini kuja mjini. Hali zinaendelea kujitokeza

mijini zitakazofanya iwe vigumu sana kwa wale wa imani yetu kuendelea kubaki humo. Kwa hiyo,

lingekuwa kosa kubwa sana kuweka fedha zetu katika ujenzi wa shughuli za kibiashara mijini. -----

Manuscript 76, 1905.

Kuishughulikia Miji Kutoka Katika Vituo Vya Mbali

Kwa kadiri inavyowezekana, taasisi zetu zingejengwa mbali na miji. Hatuna budi kuwa na

watenda kazi kwa taasisi hizo, na iwapo zinajengwa mjini, hiyo humaanisha kwamba watu wetu

hawana budi kukaa karibu nazo. Lakini si mapenzi ya Mungu kwamba watu wake wakae mijini

ambamo mna ghasia nyingi [makelele] na machafuko. Watoto wao na waepushwe na hali hiyo;

maana mfumo mzima wa mwili huathirika kitabia kwa ghasia za kwenda huku na huko, kukimbiakimbia

ovyo na makelele. Bwana anawataka watu wake wahamie kule shamba [vijijini], ambako

watakaa kwenye mashamba yao, na kupanda matunda yao pamoja na mboga za majani, tena,

mahali pale watoto wao wanapoweza kuangalia moja kwa moja kazi za Mungu katika maumbile

[viumbe vya asili]. Nendeni na familia zenu mbali na miji ndio ujumbe wangu.

Kweli ni lazima isemwe, haidhuru kama watu wataisikia [wataizingatia], au wataikataa. Miji

imejaa majaribu mengi. Tungepanga mipango yetu ya kazi, kwa kadiri iwezekanavyo, kwa namna

ambayo tutaweza kuwazuia vijana wetu wakubwa mbali na uchafu huo.

Miji inatakiwa kushughulikiwa kutokea kwenye vituo vya mbali. Akasema yule mjumbe wa

Mungu, "Je! hivi miji hiyo haitapewa onyo? Naam; si kwa njia ya watu wa Mungu kuishi humo,

bali kwa njia ya wao kuitembelea, na kuwaonya juu ya kile kinachokuja juu ya ulimwengu huu." ---

-- Letter 182, 1902.

Mahali Pale Ambapo Ni Rahisi Kuifikia Miji Hiyo

Hebu watu wenye akili timamu wachaguliwe, sio kwa kusudi la kutangaza kile wanachokusudia

kufanya, bali kwa ajili ya kutafuta mali ya kumiliki katika maeneo yale yaliyo katika wilaya za

vijijini, mahali pale ambapo ni rahisi kuifikia miji hiyo, panapofaa kujenga shule yetu ya mafunzo

kwa ajili ya watenda kazi wetu, mahali ambapo panaweza kujengwa huduma za kuwatibu watu na

kuwahudumia wale wasioijua kweli. Tafuteni mahali kama hapo nje tu ya miji mikubwa, mahali

ambapo majengo yanayofaa yanaweza kupatikana, aidha kama zawadi toka kwa wenye majengo

hayo, au kwa kuyanunua kwa bei nzuri kutokana na misaada ya fedha iliyotolewa kwa hiari toka

kwa watu wetu. Msijenge majengo katika miji hiyo iliyojaa makelele mengi. ----- Medical

Ministry, uk. 308,309. (1909).

Mafundisho Toka Kwa Henoko na Lutu

Sisi kama watu wake Mungu wanaozishika amri zake [kumi] ni lazima kuihama miji. Kama vile

alivyofanya Henoko, hatuna budi kufanya kazi yetu [ya kuongoa roho] mijini, lakini tusikae humo.

----- Evangelism, uk. 78,79. (1899)

Maovu yanapozidi sana katika taifa lo lote lile, daima husikika sauti fulani inayotoa onyo na

mafundisho, kama vile sauti ya Lutu ilivyosikika kule Sodoma. Hata hivyo, Lutu angeweza

kuiokoa familia yake kutokana na maovu yale mengi, kama asingalikuwa amefanya makazi yake

katika mji ule mwovu, ambao ulikuwa umejaa uchafu mwingi. Mambo yote ambayo Lutu na

familia yake walifanya mle Sodoma wangeweza kuyafanya hata kama wangeishi mahali fulani

mbali kidogo na mji ule. Henoko alitembea na Mungu, lakini hakukaa katikati ya mji wo wote

uliochafuka kutokana na kila namna ya vitendo vya kikatili vya kutumia nguvu pamoja na uovu,

kama Lutu alivyofanya kule Sodoma. ----- Evangelism, uk. 79. (1903)

Makanisa, Ila Sio Taasisi, Kuwamo Mijini

Tena na tena Bwana ametuagiza sisi kuwa inatupasa kuishughulikia miji kutokea kwenye vituo

vyetu vilivyo mbali. Katika miji hiyo hatuna budi kuwa na nyumba zetu za ibada [makanisa], kama

kumbukumbu za Bwana, lakini taasisi za kuchapisha vitabu vyetu, za kuponya wagonjwa, na zile

za kuwafundisha watenda kazi wetu; zinapaswa kujengwa nje ya miji. Hasa ni muhimu kwamba

vijana wetu waepushwe na majaribu ya maisha ya mjini.

Inapatana na agizo hilo, kwamba nyumba za kukutania [makanisa] zimenunuliwa na kuwekwa

wakf katika mji wa Washington na Nashville, ambapo nyumba za uchapishaji na hospitali zilizo

katika vituo hivyo zimejengwa mbali na sehemu za katikati za miji hiyo yenye msongamano wa

watu wengi sana, kama vituo vya kazi vilivyo mbali na mji. Huo ndio mpango uliofuatwa katika

kuziondoa nyumba nyingine za uchapishaji pamoja na hospitali na kuzijenga mashambani [vijijini],

na jambo hilo linafuatwa kule Uingereza kwa habari ya nyumba ya uchapishaji ya London pamoja

na shule ya mafunzo iliyopo pale. Hivi sasa tumepewa nafasi ya kusonga mbele kwa maongozi ya

Mungu yaliyofunuliwa kwa njia ya kuwasaidia ndugu zetu katika vituo hivyo muhimu na

vinginevyo kwa kuanzisha kazi yetu juu ya msingi ulio imara, ili ipate kuendelezwa mbele kwa

uthabiti. ----- Special Testimonies, Series B, No. 8, uk. 7,8. (1907)

Tunatakiwa kuwa na busara kama nyoka na wapole kama hua katika juhudi zetu za kutafuta mali

ya kumiliki kule shamba [vijijini] kwa bei ya chini, na kutoka kwenye vituo hivyo vya mbali

tunapaswa kuihudumia miji hiyo. ----- Special Testimonies, Series B, No. 14, uk. 7. (1902)

Ujumbe Tuliopewa na Bwana

"Tokeni mijini; tokeni mijini!" ----- huo ndio ujumbe alionipa Bwana. Matetemeko ya nchi

yanakuja; mafuriko yanakuja; sisi hatutakiwi kujijenga katika miji hiyo miovu, ambamo yule adui

[Shetani] anatumikiwa kwa kila njia, na ambamo Mungu mara nyingi anasahauliwa. Mungu

anataka tuwe na macho safi ya kiroho. Yatupasa kuwa wepesi kutambua hatari kubwa ambayo

ingeweza kuambatana na ujenzi wa taasisi zetu katika miji hiyo miovu. Yatupasa kupanga mipango

yetu kwa busara ili kuionya miji hiyo, na wakati uo huo kuishi mahali pale tunapoweza kuwakinga

watoto wetu pamoja na sisi wenyewe dhidi ya mivuto ile michafu inayoharibu tabia ambayo

imeenea sana mahali hapo. ----- Life Sketches, uk. 409, 410. (1906)

SEHEMU YA TISA

Kukimbia Wakati wa Hatari Mwishoni mwa Pambano Hilo

Ishara ya Kuanza Kukimbia

Huu sasa sio wakati kwa watu wa Mungu kuendelea kuyakaza mapenzi yao au kujilimbikizia

hazina zao katika ulimwengu huu. Wakati hauko mbali, ambapo sisi, kama wanafunzi wale wa

mwanzo [wa Yesu], tutalazimika kutafuta kimbilio letu maporini na mahali pasipo na watu. Kama

vile kule kuzingirwa kwa Yerusalemu na majeshi ya Warumi ilivyokuwa ishara ya kukimbia kwa

Wakristo wale wa Yudea, hivyo ndivyo, kule kujitwalia madaraka kwa upande wa taifa letu [la

Marekani] kwa njia ya kutunga amri ile inayowalazimisha watu wote kuitunza sabato ya papa

[Jumapili], kutakavyokuwa onyo kwetu sisi. Wakati huo ndipo saa itafika ya kuondoka katika miji

mikubwa, tukijiandaa kuihama miji midogo ili kwenda mafichoni kwenye makazi yale ya upweke

katika milima. Na, kwa sasa, badala ya kutafuta hapa [duniani] makazi yaliyojengwa kwa gharama

kubwa, tungekuwa tunajiandaa kuhamia kwenye nchi ile iliyo bora, yaani, ile ya mbinguni. Badala

ya kutumia fedha zetu kwa kujifurahisha nafsi zetu, tungekuwa tunajifunza kubana matumizi

[kutumia fedha zetu kwa uangalifu sana]. ----- Testimonies, Gombo la 5, uk. 464,465. (1885)

+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++

MWISHO

+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++

JIPATIE VITABU HIVI VIPYA KABISA!

Vitabu vipya kadhaa vimekwisha kuchapishwa na vingine vimo mbioni kuchapishwa. Wasomaji

wanaotaka kujua habari zaidi pamoja na bei za vitabu hivyo wanaombwa kuandika barua zao kwa

Leaves of Life International, P.O. Box 17, MAFINGA, Tanzania:-

1. KRISTO NA HAKI YETU, na E. J. Waggoner.

Kitabu hiki ni muhimu kwa kila Mkristo anayetaka wokovu ili awe tayari kumlaki Yesu

hewani.

2. UPONYAJI WA MUNGU, na Mary Ann McNeilus, M.D.

Kitabu hiki ni muhimu kuwa nacho. Punguza gharama za matibabu kwa kutumia njia 8

rahisi ambazo hazigharimu fedha. Epukana na magonjwa yasiyokuwa ya lazima. Jifunze

matumizi ya maji na mkaa kwa tiba rahisi za kushangaza.

3. MWITO WETU MKUU, na E. G. White.

Kitabu cha kesha la asubuhi kwa mwaka mzima. Kila robo mwaka ina kijitabu chake.

Robo nne hufanya kitabu kizima cha kudumu. Usizitupe. Tunza kwa matumizi ya kila

mwaka.

4. MNYAMA, JOKA, NA MWANAMKE, na Joe Crews.

Unabii unaolinganisha Pembe Ndogo ya Danieli 7 na Mnyama kama Chui wa Ufunuo 13.

Ni nani huyo? Ana athari gani kwako na kwa ulimwengu mzima? Usikikose kujipatia

kitabu hicho.

5. TOKA SABATO KWENDA JUMAPILI, na Carlyle B. Haynes.

Kitabu ulichokuwa ukikihitaji ili kujibu hoja zako zote juu ya Sabato na Jumapili.

Mabadiliko ya kalenda, sabato za kivuli, na kadhalika. Utunzaji wa Jumapili

ulivyoanza pamoja na semi mbalimbali za Viongozi wa Kiprotestanti juu ya Sabato.

6. UGONJWA NA SABABU YAKE, na E. G. White.

Kwa nini wanadamu wamedhoofika na wanazidi kudhoofika hivyo? Kwa nini ni vibaya

sana kuoana watu waliopitana umri kwa miaka mingi sana? Kuna madhara gani? Kwa

nini madawa ya kisasa ambayo ni sumu sio suluhisho kwa tiba halisi ya mwili? Usikose

kujipatia kitabu hiki.

7. IMANI NA MATENDO, na E. G. White.

Wengi wamechanganyikiwa kuhusu fundisho hilo la imani na matendo. Na wengi

watapoteza wokovu wao kwa kutokuwa na hakika juu ya mambo hayo mawili.

8. SIKU YA BWANA, na R. J. Wieland.

Kuna utata mkubwa kuhusu Siku ya Bwana miongoni mwa Wakristo. Wengine

wanadhani ni Jumapili, na wengine wanadhani ni Jumamosi. Biblia yasemaje?

Mwandishi huyu amelifafanua suala hili kwa njia rahisi kabisa.

9. MSALABA NA KIVULI CHAKE, na Stephen N. Haskell.

Somo la Patakatifu limeelezwa kwa njia rahisi sana inayoeleweka kwa mtu wa kawaida.

Huduma ya hekalu la duniani ilikuwaje? Huduma ya hekalu la mbinguni ikoje? Wokovu

wako unaathiriwaje na huduma ile ya mbinguni? Yesu anafanya nini sasa mbinguni?

Maswali hayo yanajibiwa. Sabato 7 za kivuli zaWakolosai 2:16,17 zimefafanuliwa humo.

10. HATARI KUBWA MBELE YETU, na Robert W. Olsen.

Matukio ya kutisha ya siku za mwisho yameelezwa waziwazi humo. Usikose kukinunua.

VITABU ZAIDI VINAANDALIWA KWA AJILI YAKO.


Nilikusudia jambo, hili ndilo fundisho nililotamani sote tulipate. Nimefikia mwisho wa muendelezo wa chapisho la kitabu kiitwacho TOKENI MIJINI. Kwa kuzingatia umuhim wa huduma katika jamii…sina budi kumshukuru Mungu kwa kunifungua mawazo kwa msaada wa www.swahilitruth.com. Tupo pamoja katika kila hali.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni