Mtayarishaji

Morning Star Radio

Jumapili, Januari 02, 2011

MUZIKI WA INJILI VIPENGELE VYA KIHISTORIA
kwa kuanza nitaanza na uchambuzi wa mtindo wa muziki wa Injili 'Gospel' na hii ni hatua nyingine ya mfululizo wa uchambuzi wa kina wa mitindo mbalimbali ya muziki hapa duniani leo tutiririke katika mtindo huu wa kiimani zaidi kama nilivyowagusia wiki iliyopita, hasa juu ya fungamano zake na imani ya Kikristu.

Mitindo ya kiimani ipo mingi, siku za usoni kadri tutakavyopata nafasi tutaweza kuichambua na hiyo mingine pia, hii ni mitindo kama ya Bingi ambayo ni ngoma ya kuabudia ya kirastafari, Quasida, inayohusika sana na Uislamu.

Mbali na hilo pia ipo mathalan, mitindo ya kuimba ya imani lukuki duniani kama vile Bhudha, Hare Krishna na hata imani za Kihindu, ambayo muziki wake pia una mchanganyiko na muziki wao wa kienyeji kama ule uliokuwa ukipigwa na gwiji wa mtindo huo aliyefariki hivi huko India akiwa na umri wa miaka tisini na moja, Ustaa Bismilkhan.

Ustaa Bismilkhan aliyekuwa akipiga Classicalâ za Ki-hindu kwa takriban miaka sabini na tano, tangu alipokuwa na miaka kumi na sita na tutayaona siku za mbeleni panapo majaliwa, kwa sasa tujikite katika mtindo wetu huu wa Gospel 'miondoko ya kumsifu Mungu'.Sina shaka nikikutajia jina unajenga picha ya haraka ya wasanii waliojizolea umaarufu mkubwa sana kwa sasa katika muziki huu.

Kwa hapa nyumbani hawa ndio mastaa wetu wa muziki huu kwa nyakati hizi japo kihistoria kabla ya hapo kulikuwa na watu waliotamba katika anga hizi, baadhi ya wanamuziki waliotamba katika muziki wa kidunia na baadaye kuingia kwenye Gospel.

Hivi ni nini hasa maana ya jina la muziki huu, kwa lugha ya Kiingereza linalotamkwa Gospel? Wengi huuita mtindo huu kwa Kiswahili kama Muziki wa kumtukuza Mungu au Muziki wa Injili

Yote haya yako sawa, lakini katika namna tofauti na uelewa wa wengi wetu, tafsiri ya neno la Kiingereza Gospel kwa Kiswahili ni mafundisho matakatifu ya neno la Mungu katika maandiko yake yanayopatikana katika kitabu kitakatifu cha Biblia.

Mengi zaidi yakihusisha Agano jipya na mafundisho ya Bwana Yesu Kristo, kama yanavyosimuliwa katika injili nne zilizoandikwa na Mathayo, Marko, Luka na Yohana.

Neno Injili linalomaanisha Habari Njema linatokana na neno la Kigiriki Eungelion.

Katika hilo hilo agano jipya zaidi ya injili hiyo iliyoandikwa mara nne huku tatu zikifanana sana kwa ukaribu, kuna mafundisho pia ya Mtume Paulo hasa kupitia nyaraka zake mbalimbali.

Kama nilivyoeleza hapo awali, ni sahihi kwa muziki huu kuitwa wa Injili na wa kumtukuza Mungu pia kwa maana ya kupitia Injili hiyo ya Yesu.

Lakini kwa maana halisi ya mwanzo wa neno la Mungu ambalo lilianza katika Agano la Kale linaloanza na kitabu cha Mwanzo, kabla hata hawajazaliwa manabii waliokuja kubashiri kuzaliwa kwa Masihi.

Hiyo ina maana gani? Kwamba Mungu alianza kuimbiwa na kutukuzwa mara baada ya kumaliza kazi ya kuumba dunia kabla ya kumuumba binadamu.

Maana viumbe vingi alivyoviumba wakiwamo wanyama, miti, ndege, pepo vyote vilitoa sauti na kuimba katika namna yake na kutimiliza utukufu wake.

Msikilizaji, kimsingi muziki unaundwa na sauti kwanza na usipate dhana kwamba ni vyombo, vyombo havitaweza kujenga msingi wa kuundwa kwa muziki kama hakuna sauti na ndio maana vyenyewe vimetengenezwa kutoa sauti.

Lakini kama tunafuata msingi wa maandiko, sauti za kwanza kuwepo duniani ni hizo za viumbe nilivyovitaja kabla ya kuumbwa Adam.

Ukisoma katika Agano la Kale, unaona pia kutukuzwa kwa Mungu katika kitabu cha Kutokaâ 15:1-18 na 19:20:21 hizi zikiwa ni nyimbo za kumsifu Mungu baada ya kuwakomboa wana wa Israel kutoka utumwani huko Misri.

Zipo pia nyingine alizoimbiwa kutokana na mema yake, kama katika kitabu cha Samuel (2):6:5 na 22:2-51 alizoimbiwa na Mfalme Daudi na pia katika kitabu cha Isaya 26:2-19.

Mbali na hizo zipo nyingi sana katika maandiko kwa nyakati na nafasi mbalimbali, kwanini inatupasa kuyajua yote hayo? Ni kwa sababu muziki huu wa kumtukuza Mungu unatokea mbali sana kulikoni unavyoweza kuufikiria.

Katika kukutayarisha kabla hatujaanza uchambuzi rasmi, naomba nikugusie kuwa tutasafiri kiuchambuzi tangu kuanza kuumbwa kwa ulimwengu na tutapitia nyakati hizo za Agano la Kale, tutakuja katika zama za masinagogi na wakati wa Yesu na tutapitia pia katika Ukristo na kuanza kwa kanisa.

Tutachambua kuanza kwa madhehebu na mgawanyiko wake kulikosababisha kuzaliwa kwa mirindimo tofauti ya kikanisa kutokana na hilo.

Tukitoka hapo tutaelekea katika mitindo mbalimbali ya kimuziki katika hiyo ya Gospel usishangae maana kuna hadi Hip Hop za ki-Gospel eti!!!.

Tutajikita pia katika Modern Gospel na nguvu ya muziki huu katika soko la kibiashara, kama ilivyo kwa Biblia kuwa ni kitabu kinachouza sana na hatimaye tutaperuzi madai ya baadhi ya wadau wa muziki.

Kwamba huu ndio mtindo uliokuja kuupoka ufalme wa Bongo Fleva katika anga za muziki hapa nyumbani, ACAPPELLA. Sina shaka basi utajiandaa vyema kupokea mtiririko huu maridhawa, na natazamia kupata changamoto, maoni na mengi kutoka kwako msikilizaji wa kipindi cha muziki wa acappella na msomaji wa blog hii.


Jambo hili linawalenga hasa wadau wenyewe wa muziki huu wa acappella ambao wengi wao ni wasikilizaji wa Morning Star Radio 105.3 fmDar es salaam.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni