Dawaz ni usanii wa jadi wa mchezo wa sarakasi wa kabila la Wauyghur. Maana ya "Dawaz" katika lugha ya Kiuyghur ni "kutembea kwenye kamba iliyofungwa juu". Mchezo wa Dawaz una historia zaidi ya miaka 2,000, na unapendwa sana na watu wa makabila mbalimbali wanaoishi katika mkoa unaojiendesha wa Xinjiang Wauyghur. Kikundi cha sarakati ya Dawaz cha shirika la maonesho ya sarakasi la Xinjiang ni kikundi maalumu kwa ajili ya kufanya maonesho ya mchezo wa Dawaz, na wamefanya juhudi kubwa katika kurithisha na kuendeleza usanii wa mchezo wa Dawaz, na kufanya usanii huo uwe na mvuto mkubwa duniani siku hadi siku.
Kiongozi wa kikundi hicho Bw. Adil Hoxur ni mrithi wa kizazi cha sita wa usanii wa mchezo wa Dawaz. Bw. Hoxur alizaliwa mwaka 1971 katika familia moja ya wachezaji wa Dawaz iliyoishi katika wilaya ya Yingjisha ya sehemu ya Kashi mkoani Xinjiang. Baba yake ni mchezaji maarufu wa Dawaz wa sehemu hiyo. Alipokuwa mdogo, mara kwa mara aliwasikia mama na kaka yake wakisema baba yake anaweza kufanya kitendo cha ajabu anapotembea kwenye kamba. Alisema, "Mimi na ndugu zangu tulishindwa kujifunza kitendo hicho. Baba yetu aliweza kupanda kamba iliyofungwa juu kwa pembe ya digrii 45 kwa miguu tu huku akiwa amebeba mtu, na miguu yake inashikilia kamba vizuri kama koleo. Baba yangu aliweza kufanya kitendo hicho mpaka alipokuwa na umri wa miaka 72, na mwaka huo alifanya maonesho yake ya mwisho ya Dawaz kwa wakazi wa wilaya ya Yingjisha."
Baba wa Bw. Hoxur alikataa kumfundisha Hoxur ufundi wa Dawaz, kwani alifahamu sana kuwa ni mchezo wenye hatari kubwa. Bw. Hoxur alipokuwa mdogo, hakujua sana Dawaz. Alisema, "Baba yangu alifariki dunia nilipokuwa na umri wa miaka mitano. Nilipokuwa mdogo sikujua sana Dawaz. Mama yangu aliniambia kuwa familia yangu imekuwa familia ya wachezaji wa Dawaz kizazi baada ya kizazi. Alinielezea maana ya Dawaz akichora picha kwenye ardhi, na kusema wachezaji wa Dawaz wanaweza kutembea kwenye kamba iliyofungwa juu kwa urefu wa mita 21 ardhini. Nilishagaa sana kuwa baba yangu aliweza kupanda sehemu iliyo juu namna hii, nikaamua kuiga mfano wa baba yangu na kujifunza Dawaz. Baadaye nilifahamu vizuri mchezo wa Dawaz hatua kwa hatua na kuupenda mchezo huo siku hadi siku."
Wakati wa kusherehekea sikukuu, watu wa kabila la Wauyghur hawawezi kukosa maonesho ya Dawaz. Kwa kawaida maonesho hayo yanafanyika kwenye uwanja ulio wazi, wachezaji wa Dawaz wanatembea tembea juu ya kamba inayofungwa juu kwa urefu wa mita kumi kadhaa kutoka ardhi, na kufanya vitendo mbambali. Maonesho hayo huwasisimua sana watazamaji.
Mwaka 1986, Bw. Hoxur alikwenda mjini Urumuqi kwa mara ya kwanza, na kufanya maonesho ya Dawaz kwa ajili ya wanamichezo wa Michezo ya tatu ya watu wa makabila madogo madogo nchini China. Maonesho hayo yalimfanya afahamike sana na watu wengi. Bw. Hoxur alisema, "Hii ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kufanya maonesho hadharani mbele ya watu wengi. Watazamaji hao walishangilia na kupenda sana maonesho yangu, na wengi wao walituomba kupiga picha nao. Nilitambua kuwa chaguo langu la kujifunza Dawaz ni zuri, na niliona kuwa mimi ni shujaa, naweza kufanya jambo ambalo watu wengine hawathubutu kufanya."
Ili kuendeleza na kustawisha usanii ywa mchezo wa Dawaz, mwaka 1990 serikali ya mkoa unaojiendesha wa Xinjiang Wauyghur iliwakusanya wachezaji wa Dawaz wa kabila la Wauyghur na kuunda kikundi cha maonesho. Hali hii ilitoa fursa nzuri kwa ajili ya maendeleo ya Dawaz. Mkuu wa shirika la maonesho ya sarakasi la Xinjiang Bw. Anwar Mammat alisema, "Baada ya wachezaji hao 20 wa Dawaz kujiunga na shirika letu, tulifanya kazi nyingi za kuhakikisha usalama. Dawaz ni mchezo wa jadi, ili kuufanya mchezo huo uwe na thamani kubwa zaidi ya kisanaa, tulifanya marekebisho katika mambo mbalimbali."
Zamani maonesho ya mchezo wa Dawaz yalifanyika kwenye uwanja ulio wazi, hivi sasa maonesho hayo pia yanafanyika kwenye jukwaa la opera. Katika miaka ya hivi karibuni, Bw. Hoxur pamoja na wenzake walivumbua vitendo vingi vipya vyenye hatari kubwa, vikiwemo kupanda baiskeli yenye gurudumu moja, kuvingirisha bakuli na kuruka kamba juu ya kamba.
Mwaka 1997, Bw. Hoxur alifanikiwa kupita kamba ya chuma cha pua yenye urefu wa mita 600 iliyofungwa kati ya kando mbili za Mto Changjiang katika Magenge Matatu kwa dakika 13 na sekunde 48, bila kuwekwa zana za kuhakikisha usalama, na kuvunja rekodi ya Guinness kwa mara ya kwanza. Tarehe 6 Oktoba mwaka 2000, alipita kamba ya chuma cha pua yenye urefu wa mita 1399.6 iliyofungwa juu ya Mlima Heng, bila kuwekwa zana za kuhakikisha usalama, na kuvunja rekodi ya Guinness tena. Mwaka 2002, Bw. Hoxur alikaa juu ya kamba iliyofungwa juu ya ziwa Jinhai huko Pinggu kitongoji cha Beijing kwa siku 25. Jambo hilo lilifuatiliwa na dunia nzima, na alisifiwa kuwa "Mfalme wa Anga ya Juu" wa China.
Mafanikio hayo ya Bw. Hoxur yamewafanya watu wengi zaidi wafahamu usanii wa mchezo wa Dawaz. Hivi sasa sanaa hiyo ya kabila la Wauyghur imewekwa kwenye orodha ya mali za urithi wa utamaduni usioonekana ya China. Wakati huo huo shirika la maonesho ya sarakasi la Xinjiang pia linajitahidi kufundisha wachezaji wengi zaidi wa mchezo wa Dawaz. Bw. Hoxur na wanafunzi wake wanaimani kuwa mchezo huo utarithishwa kizazi baada ya kizazi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni