Mtayarishaji

Morning Star Radio

Jumatatu, Desemba 20, 2010

BARAZA LA SANAA TANZANIA


Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), liko mbioni kuachia mikakati mizito ya kukuza sekta ya sanaa hapa nchini Tanzania ikiwiwa ni pamoja na kujenga jumba la sanaa litakalokuwa na hosteli za wasanii kwa ajili ya kuishi wakati wakiandaa kazi zao za sanaa.

Akizungumza Katibu Mtendaji wa BASATA jijini Dar es Salaam Ghonche Materego alisema ya kwamba, lengo la nyumba hiyo ya sanaa ni kuwatengenezea sehemu ya eneo maalumu kwa ajili ya wasanii ili wawe na mahali pazuri pa kuandalia kazi zao na kufanya maonyesho.

Mbali na jumba hilo la sanaa, Materego aliongeza kwa kusema kwamba, BASATA iko kwenye hatua za mwisho za kukamilisha ukumbi mkubwa na wa kisasa wa sanaa na burudani wenye uwezo wa kuingiza watu zaidi ya 1,000 wakiwa wamekaa, ambao unatarajiwa kwamba utafufua rasmi sanaa za maonyesho ya jukwaani, ambazo zimekuwa katika hatari ya kutoweka kutokana na kukosekana kwa eneo maalum la kuzionesha na kuziuza.

“Ni matarajio ya Baraza la sanaa Tanzania kwamba, nyumba na ukumbi huo wa sanaa na burudani ulio katika hatua za mwisho utakapokamilika, kutakuwa na uhai mkubwa wa sekta hii hapa nchini, kiasi cha kuanza kuamsha ari na pia kumeesha mizizi kwa Watanzania wengi hususan wale ambao hawathamini sanaa za nyumbani kwao.”

Akizungumzia suala la haki na wizi wa kazi za wasanii, Materego alisema kwamba, pamoja na kuwepo mamlaka nyingine inayoliangaza jambo hilo, BASATA katika mipango na mikakati yake inakusudia kuunda kitengo maalumu cha kulifuatilia, hasa kwenye sanaa za asili ili kuhakikisha tatizo la wizi za wasanii zinapungua na kuimarisha kipato cha wasanii.

Aidha, Materego alieleza zaidi kwamba, muda umefika sasa wa kuwepo kwa sera ya sanaa inayojitegemea, badala ya ilivyo sasa, ambako sekta hiyo inayokua kwa kasi na kuwa tegemeo la vijana wengi.

“Baraza linakusudia kushawishi kupitia njia mbalilmbali, ili sera ya taifa ya sanaa iundwe na baadaye kuleta mageuzi makubwa katika tasnia hii.

Hakuna sababu ya sekta ya sanaa kufichwa ndani ya sera ya utamaduni, kwani kwa sasa imekua sana na kuhitaji muongozo huru wenye kuhitaji uratibu wa kitaifa wa moja kwa moja,” hapa alisisitiza kweli kweli.

Alizidi kusema kwamba, pamoja na sekta ya sanaa hapa nchini kuongozwa na sera ya utamaduni ya mwaka 1997, bado sheria za Bunge na zile ndogondogo zinazosimamia sekta hii ni za 1984, hali inayohitaji kufanyiwa marekebisho makubwa.

Baraza la Sanaa la Taifa ni shirika la umma lililoundwa kwa sheria ya Bunge namba 23 ya mwaka 1984 na kazi zake kubwa ni kuratibu matukio ya sanaa nchini, kusimamia na kukuza sekta ya sanaa nchini kupitia kuhimiza ubunifu wa sanaa bora asilia.

Sasa, kazi kwako mwana sanaa.

Maoni 1 :

  1. tunashukuru basata kwa kukuza sanaa yetu tanzania ila ina maana wanaokodisha cd na kuuza cd wauzaji hawa wadogo wadogo wamesha anza kulipia kodi ya wasanii kama bado basi huku tanga tumesha ambiwa waanza kulipia kila mmoja 75 elfu halafu inaelekea haiko offical kwani siinge tangazwa nchi nzima iweje ni tanga tu.

    JibuFuta