Katika jitihada yao yote ya kufafanua na kuelezea taaluma ya fasihi, kuna misingi kadhaa ambayo wengi huikubali au huelekea kuikubali, au wasingeipinga kama ingewekwa wazi zaidi.
Ukiitazama fasihi kwa umbo lake la nje na umbo lake la ndani utaona kuwa ni taaluma inayojengwa na maneno, na maneno yenyewe hutumia fani maalum za aina mbalimbali kutolea makusudi au maudhui ambayo humzingatia binadamu maishani. Kama vile mshitakiwa awezavyo kutoka katika hatia, japo awe mkosaji, kwa kutumia ufundi wa maneno, na kama vile awezavyo kuingia hatiani na kuadhibiwa, japo awe si mkosa, kwa utumiaji wa maneno, vivyo hivyo kufanikiwa au kutofanikiwa kwa fasihi kumo katika utumiaji wa maneno. Kwa ajili hii kushughulikia fasihi, kwa upande mmoja, ni kuhusika na kuchunguza maneno.
Utaona kuwa nimesema “kwa upande mmoja”. Hivyo si kila neon au maneno ni kazi ya fasihi ingawa mwanafasihi huweza pia kujifunza mengi yaliyomo ndani ya maneno matupu. Mfano wake ni kama ule wa mtu awezavyo kujifunza kitu kwa upumbavu wa mpumbavu, akaweza kudai kuwa hakuna upumbavu ulio upumbavu mtupu na kuwa, hata ndani ya upumbavu, mna hekia ambayo mwenye hekima aweza kujifunza.
Tusemapo fasihi hujengwa kwa maneno, lazima maneno hayo yawe ni maneno zaidi ya maneno mengine. Fasihi si kuwa na maneno ya kisanaa, bali ni kutumia maneno ya kila siku kisanaa. Katika fasihi, japo jambo lielezwalo huwa ni la kawaida, lakini umbo lake hujitokeza kwa uzuri na urembo kwa kuyatumia kisanaa maneno yayo hayo ya kawaida.
Japokuwa sanaa hii ya fasihi mara nyingine huzungumzia vitu, lakini hilo ni umbo lake la nje tu. Umbo lake la ndani hasa hujishughulisha na binadamu na ubinadamu wake maishani. Yaani binadamu ndiye kiini cha fasihi; ndiye shabaha yake. Binadamu ndiye mwanzo ndiye mwisho wa fasihi.
Fasihi humtazama binadamu na uhusiano wake na binadamu wenziwe, na mazingira yake, na viumbe vingine, na itikadi yake kuhusu mambo ya kiroho kama pepo, maruhani, mashetani, majini na MUNGU. Humzingatia binadamu katika hali yake, ya furaha na huzuni, raha na taabu, shida na mashaka. Humzingatia katika hali ya upweke na hali ya kuchanganyikika na wengine. Humfunulia huluka mbalimbali za kibinadamu, na matokeo ya huluka hizo maishani. Humfunza, humwonya, humgutusha, humsisimua, humtumbuiza na pia kumwia dhamiri dhammirini mwake huyu binadamu.
Fasihi humtizama binadamu na mazingira yake, na humtazamisha hayo mazingira yake ili ayaone. Hapo humwangalisha na kumfikirisha ili aweze kuyabadilisha mazingira, tabia na hali ya mambo ilivyo kwa manufaa yake na kuweza kumwendeleza mbele katika maendeleo yake kiuchumi, kisanaa, kisiasa na kijamii.
Fasihi humzingatia binadamu katika uwezo na udhaifu wake; kufanikiwa na kushindwa kwake; katika uvumilivu na kukata tama kwake. Na kila wakati humpa nafasi ya kujirekebisha ili awe mtu bora zaidi katika utu wake kati ya jamii, nay eye mwenyewe akiwa sehemu ya jamii yake.
CHANZO CHAKE
Chanzo cha fasihi ni hisi, ya mtu mmoja au watu katika jamii. Hisi za binadamu hujitokeza katika njia nyingi: kwaa vinyago, kwa ujenzi, kwa vifaa, zana, ususi, kilimo, ufundi, uongozi, siasa, kwa njia za uchumi na kumiliki mali, na hata kwa ngoma. Lakini hisi zitupazo fasihi ni zile zinazojitokeza katika lugha.
UKUBWA WAKE
Kama vile ambavyo hakuna aujuaye ubinadamu wote, vivyo hivyo ni vigumu kujua hisi zote, na kwa hivyo kuimiliki fasihi. Ni vigumu kumpata bingwa kwa maana hasa ya ubingwa katika kazi ya sanaa ya fasihi, hata kati ya hao wataalam wa fasihi. Fasihi kina chake katika kumzingatia binadamu ni kirefu; tena ina upana wa kiasu cha kuwapa uhuru wa kuranda wasanii na wataalamu wayo. Ama urefu wake ni vigumu kuuona mwisho au mwanzo wake.
FASIHI NA UTAMADUNI
Kutokana na ufafanuzi huu mfupi wa kijumla, tunaweza kusema kuwa fasihi ina uhusiano mkubwa na utamaduni. Maana kati ya vipengele vya utamaduni kimoja ni lugha. Lugha kama sehemu ya utamaduni ina yabia ya kuwapambanua watu. Japo siku hizi kuna jitihada ya watu kujifunza lugha mbali mbali, lakini lugha ya kujifunza haiwi yako, na mara nyingi wenyeji wa lugha hiyo uliyojifunza huweza kujua kuwa wewe si mmoja wao.
Hii ndiyo sababu leo Afrika tunasema kuwa ni vyema kujua lugha mbali mbali za kigeni katika kujenga uelewano, lakini hata hivyo ni vyema zaidi kutotegemea lugha ya kigeni kuwa lugha ya taifa. Heri kila nchi Afrika ijichagulie lugha ya Kiafrika kuwa lugha ya taifa. Tanzania, Uganda na Kenya, zote zimeamua Kiswahili kiwe lugha rasmi na lugha ya taifa. Zaire hivi sasa imo mbioni; na ingefaaa zaidi kama nchi nyingine zingeamua kutumia lugha moja ya kienyeji kuwa lugha yao ya taifa. Ni kweli uamuzi huo si rahisi, lakini ni muhimu sana.
Kwa kuwa lugha ni kipengele kimojawapo cha utamaduni, na kwa kuwa fasihi hutumia lugha, basi fasihi na ni sehemu ya utamaduni. Na iwapo utamaduni ni utashi na uhai wa taifa, ni mti wa mgongo wa taifa, basi hapana budi fasihi nayo kuwa sehemu ya uhai na utashi wa taifa hilo.Fasihi (na maelezo haya yaweza kuingia katika fasihi kwa jumla, fasihi maandishi na fasihi simulizi) si sehemu tu ya utamaduni, bali ni chombo cha utamaduni pia. Ndiyo chombo cha kukuzia, kuhifadhia, kuendelezea na kuelezea huo utamaduni. Ni chombo cha pekee kati ya taaluma mbali mbali za utamaduni. Hutokea hivyo kwa kuwa taaluma hii huhusika na jinsi lugha inavyosema na jambo linalosemwa. Kwa hivyo hutoa tafsiri mbali mbali ambazo pengine taaluma zingine hushindwa kuzitoa.